Na mwandishi wetu
Yanga imeendelea kuchanja mbuga katika Ligi Kuu NBC baada ya kuinyuka KMC mabao 3-0 katika mechi iliyopigwa leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Ushindi huo unaifanya Yanga kuendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikifikisha pointi 43 katika mechi 16 na kuwaacha mahasimu wake Simba wanaoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi saba ingawa Simba imecheza mechi 15.
Yanga iliandika bao la kwanza katika dakika ya kwanza tu ya mchezo huo lililofungwa na Mudathir Yahya baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la KMC.
Mpira uliozaa bao hilo ulitokana na kosa la kipa wa KMC, Wilbol Maseke aliyejichanganya wakati wa kuokoa na mpira ambao aliupiga vibaya na kumkuta Pacome Zouazoua na hatimaye KMC wakajikuta wakiadhibiwa mapema.
Bao hilo lilidumu kwa kipindi chote cha kwanza kabla ya Mudathir kuandika bao la pili katika dakika ya 53 safari hii akiitumia pasi ya Nickson Kibabage.
Dakika sita baada ya kupika bao hilo, Kibabage kwa mara nyingine, alimuunganishia pasi, Pacome ambaye aliifungia Yanga bao la tatu na la mwisho kwa timu hiyo.
Yanga katika mechi hiyo ilimtumia mshambuliaji wake mpya Joseph Guede ambaye aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Clement Mzize lakini hakuweza kuwafurahisha mashabiki wa timu hiyo baada ya kutoka uwanjani bila ya bao.
Matokeo hayo yanakuwa ni kipigo kingine kikubwa kwa KMC ambao katika mechi ya mzunguko wa kwanza dhidi ya Yanga, walikubali kichapo cha mabao 5-0.
Katika hali ya kushangaza kipa wa KMC, Maseke alijikuta akipambana na beki wake, Ibrahim Elias kabla ya wawili hao kuamuliwa na wenzao ingawa mwamuzi wa mechi hiyo, Omar Mdoe naye alionekana kuwashangaza baadhi ya mashabiki kwa kutotoa adhabu yoyote kwa wachezaji hao.
Baada ya ushindi huo Yanga sasa inajiandaa kuumana na CR Belouizdad ya Algeria katika mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayopigwa Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Soka KMC hoi, Yanga yainyuka 3-0
KMC hoi, Yanga yainyuka 3-0
Read also