Na mwandishi wetu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Jumamosi hii atajumuika na waandishi wa habari katika bonanza lililoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (Taswa).
Taarifa ya Taswa iliyosainiwa na katibu mkuu wa chama hicho, Alfred Mapunda ilieleza kuwa bonanza hilo litaanza saa mbili asubuhi katika klabu ya Msasani Beach na kumalizika saa moja usiku ambapo pia kutakuwa na burudani ya muziki wa dansi.
Mapunda katika taarifa yake alifafanua kuwa Waziri Mkuu Majaliwa ameridhia kuhudhuria hafla hiyo na atafika katika eneo hilo majira ya saa nane mchana.
Alisema katika taarifa yake kuwa lengo la tamasha hilo ni kuwaweka pamoja waandishi wa habari ili kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja na kuwataka waandishi na wafanyakazi wa vyombo vya habari kujumuika pamoja katika bonanza hilo.
Katika bonanza hilo waandishi pia watapata nafasi ya kushiriki katika mashindano ya michezo mbalimbali kuanzia soka, riadha, kuvuta na kuruka kamba, mpira wa kikapu, mpira wa wavu, mpira wa meza, mchezo wa vishale na mengineyo.
Bonanza hilo pia litatumika kuzindua tuzo za kila mwezi za wanamichezo bora ambazo zipo chini ya uenyekiti wa mwanahabari, Jemedari Saidi lakini pia Taswa itatumia bonanza hilo kuzindua kamati zake mbalimbali na kuzitambulisha mbele ya waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa Mapunda, Bonanza hilo linatarajiwa kuwa na waalikwa zaidi ya 2,000 wakiwamo pia viongozi wa vyama mbalimbali vya michezo na wanamichezo nguli wa zamani wa michezo mbalimbali.
Sports Mix Waziri Mkuu kushiriki bonanza la Taswa
Waziri Mkuu kushiriki bonanza la Taswa
Read also