Na mwandishi wetu
Bingwa mpya wa mkanda wa WBO Afrika, Hassan Mwakinyo amesema bado ana hamu ya kuendelea kucheza mapambano makubwa kulinda heshima yake.
Bondia huyo ameiambia GreenSports leo Jumanne kuwa kile alichokifanya katika pambano lililopita Zanzibar ilikuwa ni shauku yake ya kuwapa burudani mashabiki zake lakini bado ana hamu ya kujenga heshima zaidi.
Mwakinyo ameshinda kwa TKO pambano lake lililofanyika wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar dhidi ya bondia wa Ghana, Elvis Ahorgah.
“Bado imekuwa ni hamu yangu kubwa juu ya mashabiki zangu kufanya jambo lenye kurudisha heshima sawa na waliyonipa, naamini nitaendelea kufanya vizuri katika mapambano yajayo,” alisema Mwakinyo.
Ushindi huo umemrudisha Mwakinyo kwenye mstari baada ya kutopanda ulingoni kwa muda mrefu, hatua iliyosababisha kuendelea kushuka katika viwango vya ubora wa kimataifa lakini sasa ni dhahiri ameonesha nia ya kuhitaji mapambano zaidi.
Baada ya kurejea kutoka Zanzibar, Mwakinyo alisema yupo tayari kucheza pambano na Twaha Kassim ‘Kiduku’ iwapo watatokea watu au mapromota wa kuweka fedha nyingi kulingana na hadhi ya pambano hilo.