Abidjan, Ivory Coast
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, leo Jumapili imeshindwa kuweka rekodi ya kupata ushindi wa kwanza kwenye fainali za Afcon baada ya kujikuta ikitoka sare ya bao 1-1 mbele ya Zambia.
Katika mechi hiyo ya hatua ya makundi, Stars waliutawala vyema mchezo na kupata bao la mapema dakika ya 11 lililofungwa na Simon Msuva kwa shuti kali baada ya kuinasa pasi ya Mbwana Samatta.
Samatta, aliambaa na mpira kabla ya kumuunganishia Msuva ambaye kasi yake ilimsaidia kumzidi beki wa Zambia kabla ya kufumua shuti lililojaa wavuni mchezaji huyo kushangilia bao lake kwa staili ya kibunika sarakasi.
Stars walifanikiwa kulilinda bao hilo vyema hadi walipokutana na majanga dakika ya 88 kwa bao la kichwa la Patson Daka aliyeuwahi mpira wa kona iliyopigwa na nyota wa Simba, Clatous Chama.
Chama ambaye pamoja na nyota wa Yanga, Kennedy Musonda waliingia dakika 10 za mwisho, waliiongezea uhai Zambia na kuwatoa mchezoni wachezaji wa Stars ambao walionekana wakitumia muda mwingi kujihami.
Zambia wakifanya mashambulizi yaliyojaa umakini walilisakama lango la Stars na kupata kona mbili ya pili ikizaa bao wakati huo Stars ikitumia muda mwingi kuokoa mashambulizi.
Kabla ya kuingia mabao hayo, timu zote zilionesha uhai, Zambia katika dakika ya 31, Lameck Banda aliwapunguza wachezaji wawili wa Stars kabla ya kupiga krosi iliyompita Manula na mabeki wake na kumkuta Fashion Sakala ambaye mpira alioupiga kwa kichwa ulitoka nje ya lango.
Stars ilijibu shambulizi hilo dakika ya 33 baada ya Msuva kuambaa kwa kasi kuelekea lango la Zambia lakini akachezewa faulo na mwamuzi kuamuru upigwe mpira wa adhabu ambapo Zimbwe aliupiga vizuri na kutua kichwani kwa Bacca lakini mpira wa kichwa alioupiga ulitoka nje ya lango.
Dakika chache kabla ya timu kwenda mapumziko, Zambia ilipata pigo baada ya mchezaji wake, Kabwe Jr kupewa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu Samatta wakati wakiwania mpira wa juu.
Maofisa wa Zambia wakiongozwa na kocha wa timu hiyo, Avram Grant walilalamikia adhabu hiyo na katika mzozo huo, Grant naye akajikuta akipewa kadi ya njano.
Dakika ya 53, Zimbwe aliwatoka mabeki wa Zambia na kupiga krosi ya chinichini iliyomkuta Msuva ambaye alifumua shuti lakini mpira ulimbabatiza beki mmoja wa Zambia na kuzaa kona ambayo haikuzaa matunda.
Zambia walijibu shambulizi hilo dakika ya 60 wakitumia kosa la safu ya ulinzi ya Stars baada ya Bacca kumpasia Mwamnyeto ambaye aliumiliki mpira vibaya na kuwahiwa na Patson ambaye aliukokota na kufumua shuti la chinichini na kama si umakini wa kipa Aishi Manula, Zambia wangepata bao.
Stars ilianza kufanya mabadiliko katika kipindi cha pili kwa kuwatoa Haji Mnoga na nafasi yake kuingia Lusajo Mwaikenda na baadaye Feisal Salum ‘Fei Toto na nafasi yake kuingia Morris Abraham.
Baadaye Kibu Denis na Himid Mao nao walitolewa na kuingia Mudathir Yahya na Charles Mmombwa, mabadiliko ambayo hayakuizuia Zambia kupata bao la kusawazisha.
Kwa matokeo hayo, Stars sasa italazimika kushinda mechi yake ya mwisho katika kundi lake dhidi ya DR Congo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele lakini pia iombee Zambia isipate ushindi katika mechi yake ya mwisho dhidi ya Morocco.
Dr Congo ambayo katika mechi iliyopigwa mapema leo hii dhidi ya Morocco ilitoka sare ya bao 1-1, inashika nafasi ya pili na itaumana na Stars Januari 24.
Kimataifa Stars, Zambia zatoka sare ya 1-1
Stars, Zambia zatoka sare ya 1-1
Read also