Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema kukosa muunganiko ndio sababu ya kupoteza mchezo wa robo fainali ya Kombe la Mapinduzi kwa mabao 3-1 dhidi ya APR ya Rwanda.
Gamondi ameweka wazi kuwa baada ya kuondolewa kwenye Kombe la Mapinduzi Jumapili usiku, kitu muhimu kwao ni ubingwa wa Ligi Kuu NBC na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kocha huyo raia wa Argentina alisema ndivyo mpira ulivyo unapofanya makosa unaadhibiwa ingawa walitengeneza nafasi kadhaa kipindi cha kwanza na huenda wangeenda mapumziko na mabao mawili lakini haikuwa hivyo.
“Kipindi cha pili tuliendelea kufanya makosa, timu haikuwa na muunganiko tukaruhusu mabao mawili, bao la tatu tulilofungwa dakika tatu za mwisho ni makosa mabaya ya kupiga pasi katikati.
“Nafikiri kila mmoja ameona tulikuja hapa tukiwakosa wachezaji 13 ambao wanane wako kwenye majukumu ya timu ya taifa na watatu wakiwa wamepumzishwa na wawili wakiwa na majeraha,” alisema Gamondi.
Alisema kwenye mashindano hayo alikuwa na lengo la kuangalia viwango vya wachezaji wake ambao hawapati nafasi kwenye ligi kuu na hasa vijana waliwatumia vijana na anawapongeza kwa kazi waliyofanya.