Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba Queens, Juma Mgunda amesema pamoja na ushindi walioupata dhidi ya watani zao, Yanga Princess lakini mchezo ulikuwa mgumu kwa pande zote mbili.
Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam jana Jumatano, Simba ilishinda kwa mabao 3-1 na kupanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake (TWPL).
Mgunda alisema siri ya ushindi huo ni wachezaji wake kupambana kwa dakika zote 90 kitu ambacho kiliwapa wakati mgumu wapinzani wao Yanga.
“Mechi ilikuwa ngumu, ushindani ulikuwa mkubwa pande zote mbili, unajua utani wa jadi ndio umeongeza ushindani ndio maana hata wakishindana kuku wa Simba na Yanga basi nayo ni ‘derby’ na vita inakuwa kubwa ndani ya uwanja,” alisema Mgunda.
Naye Kocha Mkuu wa Yanga Princess, Charles Haalubono alisema kasi waliyokuwa nayo wapinzani wao Simba na mabao ya mapema ndivyo vilivyowachanganya wachezaji wake na kujikuta wanapoteza mchezo huo.
“Tumekubali matokeo tunarudi uwanja wa mazoezi kurekebisha makosa yetu, kiujumla mechi ilikuwa ngumu, wenzetu waliuanza mchezo kwa kasi na kufunga mabao mawili ya mapema sisi tulitengeneza nafasi tukashindwa kuzitumia ndio mpira ulivyo,” alisema Haalubono.