Accra, Ghana
Majina ya Thomas Partey (pichani) wa Arsenal na Tariq Lamptey wa Brighton hayamo katika kikosi cha wachezaji 27 wa Ghana kwa ajili ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazoanza baadaye mwezi huu nchini Ivory Coast.
Uamuzi wa kumuacha Partey umefikiwa na kocha wa Ghana, Chris Hughton kwa kile ambacho kocha huyo amedai kuwa mchezaji huyo anahitaji muda zaidi kupona majeraha ya misuli yanayomkabili.
“Amekuwa majeruhi, tulitarajia angekuwa katika kikosi, tunamjua ni mchezaji wa kiwango cha juu, huyu ni mchezaji ambaye amekuwa akiandamwa na majeraha,” alisema Hughton katika mkutano na waandishi wa habari.
“Nimetumia muda mwingi na Thomas pamoja na kuhusisha jopo la madaktari wa Arsenal, amekuwa na majeraha makubwa, jambo muhimu kwangu nikiwa ndiye kocha mkuu pamoja na chama cha soka ni kumpa msaada anaouhitaji katika kipindi hiki kigumu,” alisema Hughton.
Partey pia amekosekana katika kikosi cha Arsenal tangu Oktoba 8 mwaka jana wakati Lamptey yeye aliumia Novemba mwaka jana na kocha wake, Roberto de Zerbi amesema atakosekana uwanjani kwa kipinid kirefu.
Katika hatua nyingine kocha Hughton amemuita katika kikosi chake, Andre Ayew ambaye atakuwa anaweka rekodi ya kushiriki Afcon kwa mara ya nane tangu aanze kushiriki fainali hizo mwaka 2008.
Ghana, mabingwa mara nne wa Afcon wamepangwa Kundi B ambalo pia lina timu za Cape Verde, Misri na Msumbiji na watarusha karata yao ya kwanza Januari 14 dhidi ya Cape Verde.
Kikosi kamili cha Ghana kinaundwa na makipa watatu ambao ni Joe Wollacott, Lawrence Ati-Zigi na Richard Ofori.
Mabeki: Kingsley Schindler, Daniel Amartey, Mohammed Salisu, Alexander Djiku, Abdul Fatawu Hamid, Gideon Mensah, Denis Odoi, Nicholas Opoku na Alidu Seidu
Viungo: Majeed Ashimeru, Ransford Koningsdorffer, Mohammed Kudus, Richmond Lamptey, Elisha Owusu, Osman Bukari, Joseph Paintsil, Salis Abdul Samed na Baba Iddrisu,
Washambuliaji: Ernest Nuamah, Antoine Semenyo, Jonathan Sowah, Inaki Williams na Andre Ayew na Jordan Ayew.