Na mwandishi wetu
Kocha muu mpya wa Namungo, Mwinyi Zahera amesema kitendo cha kupewa nafasi kwenye timu hiyo inaonesha kuaminika na uongozi, hivyo ana kazi ya kuhakikisha timu inaendelea kufanya vizuri.
Zahera ameyasema hayo leo Jumamosi baada ya jana kutangazwa rasmi na uongozi wa Namungo kuwa kocha mpya wa kikosi chao akichukua nafasi ya Denis Kitambi aliyetua Geita Gold hivi karibuni.
“Uongozi umenipa nafasi ya kuinoa timu hii na kazi iliyonileta hapa ni kuhakikisha malengo ya timu yanafikiwa na yatafikiwa ikiwa tutafanya kazi pamoja kwa umoja na kila mtu akitimiza majukumu yake,” alisema Zahera.
Zahera amejiunga na Wauaji hao wa Kusini akitokea Coastal Union ambapo alikuwa kocha wa timu ya vijana baada ya kuondolewa kwenye kikosi cha timu kubwa.
Kocha huyo raia wa DR Congo anakuwa kocha wa tatu kufanya kazi Namungo msimu wa 2023/24 baada ya Cedric Kaze na Kitambi.
Pia Namungo inakuwa timu ya nne kwa Zahera kufundisha tangu alipotua Tanzania ambapo amepita Yanga msimu wa 2017/18, Polisi Tanzania 2022/23 na Coastal Union.
Namungo yenye pointi 17 kwa sasa iko nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC ikiwa imeshuka uwanjani mara 14, ikishinda michezo minne, sare tano na kufungwa mechi tano.