Na mwandishi wetu
Kama ilivyo Simba, Yanga nayo imefufua matumaini ya kusonga mbele katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuigaragaza Medeama ya Ghana mabao 3-0 katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Simba na Yanga zote zilikuwa zinaburuza mkia katika makundi yake na kupoteza matumaini lakini ushindi wa jana wa Simba wa mabao 2-0 mbele ya Wydad na ushindi wa leo wa Yanga dhidi ya Medeama umefufua matumaini kwa timu hizo.
Yanga iliandika bao la kwanza dakika ya 33 lililofungwa na Pacome Zouazoua ambaye alionesha juhudi binafsi na umahiri kwa kuwahadaa mabeki wa Medeama kabla ya kufumua shuti lililojaa wavuni.
Dakika ya 66 Yanga waliongeza bao la pili lililotokana na mpira wa kona uliopigwa na Yao Kouasi na kumkuta Kennedy Musonda ambaye aliupiga kichwa na Bakari Mwamnyeto kuumalizia kwa kumpoteza maboya kipa wa Medeama.
Bao la mwisho na la ushindi kwa Yanga lilifungwa na Mudathir Yahya ambaye aliujaza mpira wavuni akiitumia pasi ya Stephane Aziz Ki baada ya mabeki wa Medeama kushindwa kuumiliki mpira uliokuwa katika himaya yao.
Medeama hata hivyo kwa wakati wote walicheza kwa kujiamini kama vile ndio waliokuwa wakiongoza na walifanikiwa kutengeneza nafasi kadhaa ambazo walishindwa kuzitumia kupata matokeo mazuri.
Dakika 10 baada ya timu kutoka mapumziko, Medeama walipata penalti iliyotokana na rafu ya Bakati Mwamnyeto kwa Jonathan Sowah ambaye hata hivyo shuti lake liliokolewa na kipa wa Yanga Djigui Diarra.
Yanga ambayo ipo Kundi D, matokeo hayo yanaifanya kufikisha pointi tano huo ukiwa ni ushindi wake wa kwanza katika kundi hilo baada ya kucheza mechi nne, kutoa sare mbili na kufungwa moja.
Timu hiyo hata hivyo bado ina kazi ya kufanya katika mechi nyingine mbili zilizobaki kwa kuwa nafasi ya kufuzu robo fainali katika kundi hilo ipo wazi.
Baada ya ushindi huo uliopatikana Jumatano hii, Yanga itatakiwa kushinda dhidi ya Belouizdad ya Algeria mechi itakayopigwa jijini Dar es Salaam kati ya Februari 23 au 24 na baada ya hapo itakuwa ugenini Misri dhidi ya Al Ahly kati ya Machi 1 au 2.