London, England
Kipa wa Newcastle na timu ya Taifa ya England, Nick Pope (pichani) atalazimika kufanyiwa operesheni ya bega ambayo itamuweka nje ya uwanja kwa miezi minne.
Pope aliumia Jumamosi wakati akiiwakilisha Newcastle katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Man United na kutoka uwanjani dakika ya 86 akiwa hoi.
Katika mechi hiyo Newcastle ilishinda kwa bao 1-0 lakini kipa huyo alijikuta katika hali mbaya baada ya kuruka kuokoa shambulizi lililoelekezwa langoni mwake.
Kocha wa Newcastle, Eddie Howe alisema upo uwezekano wa kipa huyo mwenye umri wa miaka 31 kupona kabla ya kuanza kwa fainali za Euro 24 zitakazofanyika Juni mwakani nchini Ujerumani.
“Katika hali ya kawaida amekuwa mnyonge mno kwa sababu tuna mechi kubwa mbele yetu lakini pia zipo fainali za Euro zinazomsubiri, tunamfikiria sana kwa sababu ni majeruhi mwingine hatari kwetu, hapana shaka anahitaji kufanyiwa operesheni kwa hiyo atakosekana kwa kipindi fulani, tunadhani itakuwa miezi minne,” alisema Howe.
Pope anaongeza idadi ya majeruhi katika timu ya Newcastle ambayo inapambana katika EPL na Ligi ya Mabingwa Ulaya, wachezaji wengine majeruhi wa timu hiyo ni mabeki Dan Burn na Sven Botman.
Katika orodha hiyo ya majeruhi pia wamo winga Harvey Barnes na mshambuliaji Calum Wilson pamoja na viungo Jacob Murphy na Joe Willock.
Baada ya kuumia na kushindwa kuendelea nafasi ya Pope ilichukuliwa na Martin Dubravka ingawa Newcastle inadaiwa kuwa mbioni kumsajili kipa wa zamani wa Man United, David de Gea katika dirisha dogo la Januari.
Kimataifa Kipa Newcastle nje miezi minne
Kipa Newcastle nje miezi minne
Read also