Na mwandishi wetu
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limewaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’ inayoshuka dimbani Novemba 30 kumenyana na Togo.
Twiga itaumana na Togo katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa wanawake au Wafcon, michuano ambayo mara ya mwisho Tanzania kushiriki ilikuwa mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.
Twiga Stars ilitinga hatua ya mwisho ya mchujo wa kucheza mashindano hayo yatakayofanyika nchini Morocco baada ya kuwatoa Ivory Coast kwa penalti 4-2 kufuatia sare ya jumla ya mabao 2-2.
Katibu Mtendaji wa BMT, Neema Msitha, (pichani) alisema kwa niaba ya serikali anawaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi kuwasapoti Twiga kwenye mchezo huo mkubwa.
“Huu ni mchezo wa mwisho ili tupate nafasi ya kushiriki WAFCON, tuwaunge mkono hawa mabinti, tunaamini kwa sapoti ya Watanzania tunaenda kufanya vizuri.
“Tunatakiwa kuwashika mkono maana wanaenda kupambana ili kutengeneza jambo hili la kihistoria,” alisema Msitha.
Alisema milango iko wazi kwa wadau na wale wote wanaotaka kuunga mkono juhudi hizo kwa hali na mali ili Twiga ipate ushindi na kwenda kushiriki mashindano ya WAFCON.