Bujumbura, Burundi
Chama cha Soka Burundi bado kina matumaini ya kumshawishi, Nestory Irankunda kuichezea nchi yake hiyo ya asili mara baaada ya mchezaji huyo kujiunga na klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani.
Irankunda, 17, (pichani juu) alizaliwa katika kambi ya wakimbizi nchini Tanzania na kwa sasa anaishi nchini Australia na tayari ameiwakilisha timu ya taifa hilo kwenye kikosi cha vijana chini ya miaka 17.
Mchezaji huyo kwa sasa yumo katika mpango wa kwenye kikosi cha wakubwa cha Australia akiwa tayari ameitwa kwenye timu hiyo katika mechi ya kirafiki dhidi ya Ecuador mwezi Machi lakini aliishia kwenye benchi.
“Tungependa aichezee Burundi lakini yeye ndiye aliyeshika hatma yake, anaweza aje au asije kuchezea timu yetu,” alisema Rais wa Chama cha Soka Burundi, Alexandre Muyenge katika mazungumzo na BBC.
“Ana uraia wa Australia lakini wazazi wake wanatokea Burundi, Chama cha Soka Burundi kilianza kumfuatilia tangu akiwa na miaka 14 na nilipata nafasi ya kumtembelea akiwa Adelaide, tulizungumza na nilimtakia heri,” alisema Muyenge.
Irankunda mchezaji mwenye kasi, uwezo wa kupiga chenga na mashuti, Jumanne alisaini mkataba wa muda mrefu na klabu ya Bayern, mkataba ambao ataanza kuutumikia Julai mwakani.
Mchezaji huyo alijiunga na klabu ya Adelaide United ya Australia akiwa na miaka 15 na alianza kucheza ligi ya nchini humo Januari mwaka jana, hadi sasa ana mabao tisa katika mechi 39 za mashindano yote aliyoiwakilisha timu hiyo.
Kimataifa Burundi yamtaka Irankunda timu ya taifa
Burundi yamtaka Irankunda timu ya taifa
Read also