Na mwandishi wetu
Bondia wa ngumi za kulipwa Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’(pichani) anatarajiwa kupanda ulingoni Novemba 25, mwaka huu kwenye Ukumbi wa AICC, Arusha kumkabili Tshimanga Katompa raia wa DR Congo.
Pambano hilo ni la marudiano baada ya lile la awali lililopigwa Oktoba 9 mwaka juzi kwenye Ukumbi wa PTA Sabasaba, Dar es salaam ambapo Dullah Mbabe alipoteza kwa pointi za majaji wote watatu.
Pambano hilo linaloandaliwa na Kampuni ya Lady in Red Promotion chini ya Promota Sofia Mwakagenda ambaye ni Mbunge wa viti maalum mkoani Mbeya, limebeba dhima ya utalii wa ndani likiitwa ‘Boxing with Tourism’.
Kuhusu pambano hilo Mbabe anayepigana uzito wa uzito wa Super Middle alisema: “Nataka kwenda kurudisha heshima yangu ambayo niliipoteza kwa Katompa, nataka kumwambia kuwa safari hii ajiandae, sitaki kurudia makosa kama yaliyojitokeza mwaka juzi,” alisema Mbabe.
Mbali na pambano la Mbabe na Katompa ambalo ni pambano kuu, mapambano mengine ya utangulizi siku hiyo yanatarajiwa kuwa ya Loren Japhet dhidi ya Shaban Ndaro na Saleh Mkalekwa ataonyeshana umwamba na Jacob Maganga.
Ngumi Dulla Mbabe, Katompa kurudiana Arusha
Dulla Mbabe, Katompa kurudiana Arusha
Read also