Na mwandishi wetu
Kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’, Hemed Morocco amesema hakuna kundi jepesi kwenye michuano ya Kombe la Mataifa Afrika 2023 (Afcon) lakini amepata faraja kupangiwa timu ambazo wanazifahamu vizuri.
Kupitia droo iliyopangwa jana usiku katika jiji la Abidjan, Ivory Coast, Stars ilipangwa Kundi F sanjari na timu za Morocco, DR Congo na Zambia.
“Timu zote 24 zilizofuzu kucheza Afcon ni ngumu kusema ukweli na hakuna timu nyepesi au kundi jepesi japokuwa faraja kwangu ni kukutana na timu mbili ambazo mara nyingi tumekuwa tukicehza nazo na tunafahamiana hata falsafa.
“Nafikiri tuna nafasi nzuri ya kujipanga vizuri zaidi na tukafanya vema safari hii,” alisema kocha huyo muda mfupi kabla ya timu hiyo kupaa kuelekea Saudi Arabia kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan itakayocheza Septemba, mwaka huu.
Stars katika mechi mbili za mwisho dhidi ya DR Congo ilitoka sare ya bao 1-1 kabla ya kufungwa mabao 3-0, mwaka juzi kwenye mechi za hatua ya makundi kuwania kushiriki Kombe la Dunia 2022.
Zambia yenyewe ilikutana na Stars mara vya mwisho kwenye makundi ya michuano ya Chan mwaka juzi ambapo Zambia iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 na sasa inaonekana ni zamu ya Stars kujiuliza juu ya timu zote mbili, ikizingatiwa mipango na wachezaji wamebadilika katika vikosi vyote.
Mbali na hilo, mataifa hayo pia yana wachezaji ambao wanafahamiana vizuri na wachezaji wa Tanzania kutokana na ushiriki wao wa Ligi Kuu NBC.
DR Congo, Zambia
Mfano Clatous Chama wa Simba na Kennedy Musonda wa Yanga ni miongoni mwa wachezaji wa Zambia wanaotumainiwa huku wakiwa wanalifahamu vizuri soka la Tanzania kutokana na uwepo wao muda mrefu nchini.
Beki wa Simba, Henock Inonga na Fiston Mayele wa Pyramids ambaye alikuwa mshambuliaji tegemeo wa Yanga misimu miwili iliyopita nao wanaifahamu vizuri Stars na hivyo kufanya mechi za kundi hilo kuwa gumu kutokana na kufahamiana huko.

Upande wa Morocco ambayo iliweka rekodi ya kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia 2022, ilikutana na Stars mara ya mwisho 2013 kwenye kuwania kushiriki Kombe la Dunia 2014 ambapo kila timu ilishinda nyumbani kwake.
Katika mechi ya kwanza ya Kundi C, Stars ilishinda mabao 3-1 kisha mechi ya marudiano ikalala kwa mabao 2-1. Stars pia itakutana na Morocco Novemba, mwaka huu na Machi, mwakani katika mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026.
Hata hivyo, wadau wa soka nchini wanaamini Stars inaweza kufanya vizuri kama ikizingatia baadhi ya maeneo ingawa wamekiri kundi ni gumu.
Mkwasa, Mwaisabula
Kocha wa zamani wa Stars, Charles Boniface Mkwasa alisema: “Timu ya DR Congo na Zambia ziliyumba miaka ya karibuni lakini kwa sasa wamebadilika kidogo wako katika ubora. Kila timu imefanya mabadiliko, kuna wachezaji waliochipukia kama Fiston Mayele katika kikosi cha DRC.
“Na sisi tutafute na kuwaweka kikosini wachezaji wenye kiwango cha juu na si kuchagua kwa mazoea, kisha tufanye maandalizi ya kutosha katika kipindi kilichobaki, naamini tutafanya vizuri.”
Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage alisema haoni kama kuna timu ngumu kwa kuwa timu hizo zilishacheza na Tanzania kwa nyakati tofauti hivyo kuna nafasi ya kufanya vizuri.
Alisema kinachohitajika ili kuwapata wachezaji wazuri ni kurudisha michuano ya Taifa Cup na kuwapa nafasi wachezaji wa madaraja ya chini kuonekana wanaweza kupata vipaji vizuri kama ilivyokuwa zamani.
Naye kocha Kenny Mwaisabula alisema: “Si kundi jepesi ila uwezekano wa kufanya vizuri upo kama wachezaji wataandaliwa vizuri na wenyewe kujua jukumu lao la kuipigania Taifa. Kinachotakiwa ni timu kufanya maandalizi ya kutosha na kujiandaa na kila mpinzani kwa kuwa kila mmoja ana ubora wake na shauku ya kutaka kufanya vizuri.”
Beki wa zamani wa Yanga, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ alisema hakuna haja ya kulialia kuhusu kundi hilo kwani nafasi ipo, na kwamba wachezaji wakiamua kupambana wanaweza kuipeperusha bendera ya nchi.
Alisema huu ndio muda mzuri wa kuionesha Dunia kwamba Tanzania pia inaweza, ikiwa timu itajitahidi kuonesha uwezo kwa kuvuka hatua moja kwenda nyingine pasipo kuhofia majina ya wachezaji au timu wanazokutana nazo.
Stars ilifuzu michuano ya Afcon kwa mara ya tatu tangu kuanzishwa kwake baada ya kumaliza nafasi ya pili katika Kundi F ikiwa na pointi nane, nyuma ya kinara Algeria yenye pointi 16.
Timu hiyo ambayo haijawahi kuvuka hatua ya makundi, ilishiriki michuano hiyo mara ya kwanza mwaka 1980 kabla ya kushiriki tena mara ya mwisho mwaka 2018-19.