Na mwandishi wetu
Imebainika kuwa klabu ya Yanga inatarajia kusaini mikataba minono na kampuni mbili kubwa zilizopendezewa kufanya kazi na klabu hiyo ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Kariakoo, Dar es Salaam.
Rais wa Yanga, Hersi Said (pichani) akizungumza Dar es Salaam leo Jumanne aligusia suala hilo na kufunguka kuwa kampuni hizo zimehitaji kufanya nao kazi bada ya kuvutiwa na mafanikio ya timu uwanjani na utendaji kazi wa viongozi.
“Tunakwenda kusaini mkataba na makampuni makubwa mawili katika kipindi cha wiki mbili zijazo, yamevutiwa na utendaji kazi wetu na yanatamani kufanya kazi na sisi,” alisema.
Rais huyo ambaye hakuwa tayari kuweka wazi kwa kina taarifa hizo, akitaka wadau na mashabiki wa timu hiyo kungoja wakati rasmi, alibainisha kuwa hayo yanakuja kutokana na umaridadi na utendaji kazi mkubwa wa ushirikiano katika idara zao.
Hersi aliipongeza idara ya masoko, habari na vitengo vyote vya klabu hiyo akisema kila mmoja amefanya jukumu lake vizuri hadi kuwa kwenye mafanikio makubwa kipindi hiki.
Alisema kwa sasa kuna utofauti mkubwa wa mafanikio ukilinganisha na miaka miwili iliyopita na hiyo yote ni kutokana na maboresho ambayo wamekuwa wakifanya kuanzia kwenye benchi la ufundi, wachezaji na idara zote.
Hersi alisema baada ya Yanga kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya miaka 25 mipango yao ni kuhakikisha wanafanya vizuri hatua hiyo ikiwezekana kutinga hatua ya robo fainali.
Yanga ilifanikiwa kupenya katika hatua hiyo ya kwa kuiondosha Al Merrikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 3-0. Mchezo wa ugenini ilishinda mabao 2-0 kabla ya Jumamosi iliyopita kuondoka na ushindi wa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Soka Kampuni mbili kusaini mikataba Yanga
Kampuni mbili kusaini mikataba Yanga
Read also