Na mwandishi wetu
Rais wa Singida Fountain Gate, Japhet Makau ameahidi kuwazawadia donge nono wachezaji wa timu hiyo endapo watafanikiwa kutinga hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Singida keshokutwa Jumapili itakuwa ugenini Cairo, Misri kurudiana na Future FC, huku timu hiyo ya Tanzania ikihitaji matokeo ya suluhu au ushindi kutinga makundi baada ya ushindi wa bao 1-0 ilioupata kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa wiki mbili zilizopita Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Akizungumza na kituo kimoja cha televisheni nchini humo, Makau alisema kama viongozi wamejipanga kuhakikisha wachezaji wao wanakuwa fiti kimwili na akili ili waweze kupambana na kupata wanachokihitaji ambacho ni kutinga hatua ya makundi.
“Nimezungumza na wachezaji na wenyewe wanajua ambacho nimewaahidi, nisingependa kukiweka hadharani lakini endapo tutatinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa kuitoa Future mifuko yao itapendeza,” alisema Makau.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Ufundi wa Singida, Ramadhani Nswanzurimo alisema maandalizi yao tangu watue Misri yanakwenda vizuri na wachezaji wote wameonesha utayari kwa ajili ya mchezo huo.
Nswanzurimo ambaye kwa sasa ndiye anakinoa kikosi hicho baada ya kuelezwa kocha wao, Ernst Middendorp amepata udhuru, alisema wanatambua mchezo huo utakuwa mgumu kwa wenyeji wao kutaka kupata mabao ya mapema lakini wamejipanga kucheza kwa malengo ili kuhakikisha wanawadhibiti wasiwadhurau kwa kipindi chote cha mchezo huo.
Singida ambayo inashiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza imefika hatua hiyo baada ya kuifunga JKU ya Zanzibar kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3 na katika mchezo wa mkondo wa kwanza dhidi ya Future iliibuka na ushindi wa bao 1-0, bao lililofungwa na Elvis Rupia, ikiwa ndio mechi yake ya kwanza tangu asajiliwe na timu hiyo akitokea Polisi ya Kenya.