Na mwandishi wetu
Beki Novatus Dismas Miroshi amekuwa mchezaji wa pili wa Tanzania kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya Mbwana Samatta baada ya jana Jumnne kukipiga dhidi ya FC Porto ya Ureno akiwa na timu yake mpya ya Shakhtar Donetsk ya Ukraine.
Mchezaji huyo wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ aling’ara baada ya kucheza kikosi cha kwanza cha Shakhtar kwa dakika 90 katika mchezo huo wa hatua ya makundi waliopoteza kwa mabao 3-1.
Ni mara ya kwanza mchezaji huyo kucheza katika michuano hiyo mikubwa baada ya kujiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Zulte Waregem ya Ubelgiji.
Dismas aliyeanza kwa kucheza beki wa kushoto katika mechi hiyo alionesha kucheza kwa ustadi mkubwa akijaribu kuharibu mipango ya Porto, timu yenye historia kubwa katika michuano hiyo.
Licha ya kocha wa kikosi hicho, Patrick van Leeuwen kufanya mabadiliko ya wachezaji watano lakini alimuacha Dismas uwanjani akabadilisha mfumo wa mabeki watatu na Dismas kuwa mmoja wa mabeki hao wa kati kati na kumudu vyema majukumu.
Samatta ambaye ni nahodha wa Stars, aliwahi kucheza michuano hiyo akiwa Genk ya Ubelgiji kabla ya kuuzwa Aston Villa na baadaye Fenerbahçe ya Uturuki.
Miongoni mwa waliomshuhudia mchezaji huyo katika mechi hiyo ni mchambuzi na mdau wa michezo, Shafii Dauda ambaye alisema: “Bado Mtanzania kucheza Ulaya ni ndoto kubwa, kugusa michuano mikubwa kama Ligi ya Mabingwa ni rekodi, ndicho kitu ambacho kinanyima usingizi, nilimwona Mbwana akiishika Ulaya lakini bado nakosa usingizi kwa kuwa nataka iwe kawaida, iwe mazoea watoto wetu kucheza soka Ulaya kwenye hatua kubwa.”
Kimataifa Novatus aweka rekodi Ligi ya Mabingwa
Novatus aweka rekodi Ligi ya Mabingwa
Read also