Na mwandishi wetu
Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (Taswa) kimeandaa tamasha maalum la Taswa Media Day Bonanza kwa ajili ya wadau mbalimbali wa vyombo vya habari.
Katibu Mkuu wa Taswa, Alfred Lucas Mapunda (pichani) ameeleza hayo leo Ijumaa akifafanua kuwa bonanza hilo linatarajia kufanyika Desemba 9, mwaka huu ambapo lengo lake ni kuwaweka pamoja waandishi wa kada mbalimbali nchini.
Alisema miaka ya nyuma tamasha hilo lilikuwa likifanyika kila mwaka lakini halikufanyika katika miaka ya hivi karibuni kutokana na sababu mbalimbali, hivyo uongozi ulioingia madarakani mapema mwaka huu umeona umuhimu wa kulirejesha hilo.
“Lengo ni kuwaweka pamoja waandishi wa habari katika kubadilishana mawazo na kufurahi, ni kwa ajili ya waandishi wote wa habari bila kujali ni wa siasa, michezo, uchumi, afya na mambo mengine, itajumuisha pia wafanyakazi wa vyombo mbalimbali vya habari,” alisema Mapunda.
Akifafanua zaidi Mapunda alisema kwa sasa wanafanya utaratibu wa kupata pia wawakilishi wa baadhi ya wanahabari kutoka mikoani kujumuika katika tamasha hilo litakalofanyika Dar es Salaam akiamini litakata kiu ya wanahabari ambao kwa miaka mingi hawajakaa pamoja kubadilishana mawazo.