Madrid, Hispania
Mshambuliaji wa timu ya soka ya wanawake Hispania, Jenni Hermoso (pichani) aliyepigwa busu mdomoni na rais wa Shirikisho la Soka Hispania (REEF), Luis Rubiales, amemfikisha kiongozi huyo mahakamani.
Rubiales alimpiga Jenni busu la mdomoni Agosti 20 baada ya Hispania kuichapa England bao 1-0 na kuibuka kinara wa Kombe la Dunia la Wanawake (WWC) na tayari Fifa imemsimamisha kiongozi huyo kujihusisha na soka kwa siku 90.
Kitendo cha Rubiales kimekemewa na makundi mbalimbali akitakiwa ajiuzulu lakini amegoma akidai kwamba alichokifanya kilitokana na furaha isiyo kifani baada ya kubeba taji la dunia na kulikuwa na makubaliano katika jambo hilo.
Taarifa ya waendesha mashitaka nchini Hispania ilidai kuwa, Jenni amemfikisha mahakamani Rubiales mwenye umri wa miaka 46 kwa kosa ambalo wengi wanalifahamu.
Awali ofisi ya waendesha mashitaka nchini Hispania ilizungumzia uwezekano wa kumfungulia kesi Rubiales baada ya kauli ya Jenni aliposema kwamba hakukuwa na makubaliano kati yake na Rubiales katika jambo hilo na kutaka taratibu za kisheria ziangaliwe.
Jenni mwenye umri wa miaka 33, inadaiwa aliamua kulifikisha suala hilo mahakamani Jumanne hii uamuzi ambao unamuweka kiongozi huyo katika wakati mgumu ingawa mwenyewe ameonekana kujiamini akidai kwamba hajafanya kosa lolote.
Wachezaji 81 wa timu ya wanawake Hispania wakiwamo 23 walioiwakilisha timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia, wamegoma kuichezea timu hiyo kama Rubiales ataendelea kuwa kiongozi REEF.

Timu ya wanawake Hispania inatarajia kucheza mechi za Uefa Nations Ligi dhidi ya Sweden na Switzerland, mechi zitakazochezwa Septemba 22 na 26 mwaka huu.
Mechi hizo mbili zinabaki kuwa swali gumu kuhusu hatma ya mgomo huo baada ya Rubiales kusisitiza kwamba hawezi kujiuzulu kwa kuwa hajafanya kosa lolote.
REEF tayari imemtimua kocha mkuu wa timu ya wanawake Hispania, Jorge Vilda aliyeiwezesha timu hiyo kubeba taji la dunia na nafasi yake kuchukuliwa na Montse Tome.
Vilda anatajwa kuwa mshirika wa karibu wa Rubiales na hata baada ya jopo zima la benchi lake la ufundi la timu ya Hispania kujiuzulu kwa kushinikiza Rubiales ajiuzulu, Vilda aligoma kufanya hivyo na kubaki peke yake katika nafasi hiyo.