Madrid, Hispania
Ángeles Bejar ambaye ni mama wa rais wa Shirikisho la Soka Hispania (REEF), Luis Rubiales aliyesimamishwa kwa kosa la kumbusu mshambuliaji wa timu ya wanawake, amejifungia peke yake kanisani kwa alichokiita kuwa ni mgomo wa kula kupinga madhila anayopitia mtoto wake.
Mmoja wa wanafamilia ya Rubiales alithibitisha Jumatatu hii kuwa mama huyo amechukua uamuzi huo na mgomo huo anaufanyia katika kanisa la Divine Shepherdess lililopo katika mji wa Motril, Andalusia.
Mama huyo amesema kwamba ataendelea na mgomo huo hadi pale kile alichokiita kuwa ni kukosa ubinadamu na mabaya yanayomkuta mtoto wake yatakapofikia mwisho.
Rubiales amesimamishwa na Fifa kujihusisha na masuala ya soka kwa siku 90 wakati Baraza la Juu la Michezo Hispania linataka kiongozi huyo aondolewe madarakani kwa kosa alilolifanya baada ya Hispania kuifunga England bao 1-0 na kubeba Kombe la Dunia la Wanawake (WWC).
Mara baada ya Hispania kutwaa ubingwa huo Jumapili iliyopita, wakati wachezaji wakikabidhiwa medali, Rubiales alimbusu mdomoni mshambuliaji wa timu iyo, Jenni Hermoso jambo ambalo limemuweka pagumu hadi sasa.
Rubiales hata hivyo pamoja na kusakamwa kila kona lakini amekataa kujiuzulu akidai kwamba busu alilompiga mchezaji huyo lilichangiwa na furaha isiyo kifani na mchezaji huyo aliridhia na ametishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mchezaji huyo na umoja wa wachezaji profesheno.
Kufuatia kashfa hiyo, jopo la makocha wa timu ya wanawake wa Hispania wamejiuzulu nafasi zao wakishinikiza Rubiales aadhibiwe isipokuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Jorge Valda ambaye naye ameeleza kutofurahishwa na alichokifanya Rubiales.
Katika hatua nyingine waendesha mashitaka nchini Hispania wametangaza kuanza uchunguzi wa kosa la udhalilishaji kijinsia dhidi ya Rubiales.
Kuhusu mgomo wa kula wa Mama Angeles, mama huyo amesema kwamba ataendelea kufanya hivyo usiku na mchana hadi mwanaye atakapoacha kubughudhiwa katika kadhia inayomkabili.
“Hakuna udhalilishaji wa kijinsia kwa kuwa kulikuwa na makubaliano ya pande zote mbili, hata picha zinaonesha hivyo, mwanagu hana uwezo wa kumuumiza yeyote,” alisema Mama Angeles.