Turin, Italia
Klabu ya soka ya Juventus imeondolewa katika michuano ya Ulaya msimu ujao wakati Chelsea imetozwa faini ya Dola 11 milioni na Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) kutokana na makosa mbalimbali.
Kwa adhabu hiyo, Juventus inakuwa imetolewa rasmi kwenye michuano ya Europa Conference Ligi ambayo in ya tatu kwa ukubwa katika mashindano ya klabu barani Ulaya kwa kosa la kwenda kinyume na kanuni ya matumizi ya fedha (FFP).
Juventus tayari imeadhibiwa nchini Italia kwa kunyang’anywa pointi 10 kwenye Ligi ya Serie A msimu wa 2022-23 hali iliyoifanya ikose tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2023-24 pamoja na Europa Ligi na hatimaye kuangukia Europa Conference Ligi ambako pia wameondolewa.
Kwa uamuzi huo, nafasi ya Juventus kushiriki Europa Conference Ligi sasa inaangukia kwa klabu ya Fiorentina ambayo itaanza ushiriki wake katika hatua ya awali ya michuano hiyo hapo Agosti 24.
Taarifa ya Uefa iliyopatikana Ijumaa hii ilieleza kuwa Juventus pia italazimika kulipa faini ya Dola 11 milioni kwa kwenda kinyume na kanuni ya FFP na shirikisho hilo litaendelea kuichunguza klabu hiyo na kuipa adhabu nyingine kama itashindwa kuzingatia kanuni za FFP siku zijazo.
Kwa upande wa Chelsea imetozwa faini ya Dola 11 milioni kwa kutoa taarifa zisizo sahihi katika kipindi cha kati ya mwaka 2012 na 2019 wakati klabu hiyo ikimilikiwa na bilionea wa Urusi, Roman Abramovich.
Chelsea ambaye ilibeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2012 na 2021 haikufuzu michuano yoyote ya klabu barani Ulaya kwa msimu ujao wa 2023-24.
Juventus ambayo baadhi ya viongozi wake waandamizi waling’atuka tangu kuibuka kashfa hiyo, hii si mara ya kwanza kukutana na rungu la Uefa, waliwahi kufungiwa kwenye michuao ya klabu barani Ulaya mwaka 2006 na 2008 wakihusishwa na rushwa.
Kimataifa Juventus yapigwa kibano Ulaya
Juventus yapigwa kibano Ulaya
Read also