Na mwandishi wetu
Aliyekuwa winga wa Yanga, Bernard Morrison amesema yeye ni shabiki namba moja wa winga mpya wa Yanga, Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ na anasubiri kwa hamu kuona Skudu atakavyowaonesha Watanzania vitu vya mpira ambavyo hata yeye alifundishwa na winga huyo.
Skudu aliyesajiliwa na Yanga kutoka Marumo Gallants ya Afrika Kusini amewahi kucheza na Morrison wakiwa Orlando Pirates, lakini pia wakishabihiana aina ya uchezaji, wote wakitumika kama washambuliaji wa pembeni wakiwa na chenga za maudhi na mbwembwe nyingi.
Morrison ameeleza kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii kwamba anajivunia kuhusika kumleta Skudu katika timu hiyo bila kufafanua namna alivyohusika.
“Namna furaha inavyoonekana, sihitaji kuzunguma sana kwa sasa. Nitazungumza baadaye jinsi gani ninajivunia kukuleta hapa, nenda kaioneshe Tanzania vyote uliyowahi kunifundisha. Mimi shabiki yako namba moja, nakupenda kijana wangu,” aliandika Morrison.
Morrison kuonesha kuwa amevutiwa mno na Skudu kutua Yanga, aliibuka kwenye mazoezi ya kwanza ya mchezaji huyo na Yanga akiwa amevalia jezi namba sita yenye jina Skudu akimkumbatia na kufurahi kwa kumuona.
Yanga iliachana na Morrison baada ya kumalizika kwa msimu wa 2022-23 na sasa duru mbalimbali za michezo zinafafanua kuwa raia huyo wa Ghana anatarajia kutambulishwa na Singida Fountain Gate hivi karibuni.
Soka Morrison shabiki namba moja wa Skudu
Morrison shabiki namba moja wa Skudu
Read also