Croatia
Kiungo wa Real Madrid, Luka Modric, beki wa zamani wa Liverpool, Dejan Lovren na aliyekuwa mkurugenzi wa klabu ya Dinamo Zagreb, Zdravko Mamic kwa mara nyingine wameingia matatani wakidaiwa kutoa taarifa za uwongo kuhusu mikataba yao na kukwepa kodi.
Mwaka 2018, Mamic akiwa mkurugenzi Dinamo Zagreb, alikutwa na hatia kwa makosa ya ukwepaji kodi, ubadhirifu wa mamilioni ya dola na kujipatia faida isiyo halali na kuhukumiwa kifungo cha miaka sita jela ingawa alidaiwa kutimkia Bosnia kabla ya hukumu kutolewa.
Miongoni mwa makosa aliyokutwa nayo Mamic yalihusu uhamisho wa Modric wa mwaka 2008 kutoka Dinamo Zagreb kwenda Tottenham na Lovren ambaye alihamia Lyon ya Ufaransa mwaka 2010.
Modric na Lovren wao walituhumiwa kwa kosa la kutoweka wazi malipo ya kodi katika mikataba ya mamilioni ya dola walipojiunga na klabu za soka za Ulaya.
Mahakama ya Croatia hata hivyo iliwafutia tuhuma hizo wachezaji hao wawili wakati wakiwa na timu ya Taifa ya Croatia kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 na wote walikuwa katika kikosi kilichofikia hatua ya fainali na kupoteza mechi mbele ya Ufaransa walioibuka mabingwa.
Mahakama hiyo ilidai kwamba hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani Modric na Lovren katika kashfa hiyo. Modric baadaye alitwaa tuzo ya mpira wa dhahabu kwa kuwa mchezaji bora wa michuano hiyo na baadaye kutwaa tuzo ya Ballon d’Or.
Hata hivyo habari mpya zilizopatikana jana ni kwamba waendesha mashitaka nchini Croatia wamedai kuna ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani Modric ambaye pia ni nahodha wa timu ya Taifa ya Croatia pamoja na Lovren kwa madai ya kutoa taarifa za uwongo.
Zipo habari kwamba Mamic alikuwa na makubaliano binafsi na wachezaji hao kwamba wangemlipa sehemu ya mgao ambao wangeupata baada ya kuuzwa katika klabu kubwa za barani Ulaya.
Iwapo watuhumiwa hao watakutwa na hatia kwa mujibu wa sheria adhabu yake ni kifungo cha jela kati ya miezi sita hadi miaka mitano.
Kimataifa Modric matatani kwa kukwepa kodi
Modric matatani kwa kukwepa kodi
Read also