
London, England
Kiungo na nahodha wa zamani wa England, David Beckham ameshauri staa
wa Man United, Cristiano Ronaldo aendelee kuichezea timu hiyo.
Beckham ambaye pia amewahi kuichezea Man United pamoja na Real Madrid
ya Hispania kama ilivyo kwa Ronaldo, ametoa kauli hiyo wakati huu
kukiwa na mjadala kuhusu majaliwa ya mchezaji huyo kama aendelee kuwa
hapo au aondoke.
Akitetea Ronaldo kuendelea kubaki hapo, Beckham kupitia akaunti yake
ya Twitter alisema, “Bado anafanya yale anayofanya kwa ubora, anafunga
mabao na kutengeneza mabao, hicho ndicho anachokifanya Cristiano.
Beckham aliongeza kuwa, “kwa umri wake kitu anachokifanya ni cha
kipekee, natumaini ataendelea kukifanya na natumaini atabaki kwa mwaka
mwingine mmoja au miwili.

Pamoja na sifa anazopewa Ronaldo, Man United ina wakati mgumu kwenye
Ligi Kuu England ikiwa nafasi ya sita na pointi 58 na hivyo upo
uwezekano mkubwa wa kukosa nafasi katika michuano ya Ulaya msimu ujao.
Na ingawa kwa Man United hali si nzuri lakini Ronaldo mwenye umri wa
miaka 37 amekuwa akifanya juhudi kubwa na hadi sasa ameifungia timu
hiyo mabao 24, rekodi ambayo kwa hali ya kawaida si mbaya kwa mchezaji
mwenye umri huo..
Ronaldo alitua, United mwaka jana akitokea Juventus ya Italia ikiwa ni
takriban miaka 12 tangu aondoke katika klabu hiyo na kutua Real
Madrid.