Na mwandishi wetu
Mabondia Selemani Kidunda, Mfaume Mfaume na wengine zaidi ya 10 leo Alhamisi wamepima afya zao kuelekea mapambano yao yanayotarajia kufanyika Juni 30, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Khadija Hamisi aliyeongoza jopo la madaktari waliopima afya za mabondia hao alisema miongoni mwa magonjwa waliowapima ni homa ya ini, sukari, virusi vya Ukimwi, magonjwa ya zinaa na wamefanya hivyo ili kulinda afya za mabondia wanapokuwa ulingoni.
Baada ya kumaliza kupima, Kidunda anayetarajia kuzichapa na Eric Mukadi wa DR Congo alisema yuko fiti na amekuwa na mazoezi ya kutosha kwa ajili ya kuwapa burudani Watanzania na kuondoka na ushindi.
“Nimejiandaa vizuri mpaka sasa, nina afya nzuri, nategemea pambano litakuwa zuri sana, nahitaji kuwafurahisha Watanzania, nataka kufanya kitu watu ‘wa-enjoy’, maana mchezo wa ngumi ni mchezo wa burudani, waje waangalie Kidunda anafanya kitu gani, tunaomba maombi yao pia kuelekea pambano hili,” alisema Kidunda.
Naye Mfaume Mfaume atakayepambana na Mkululeko Mhlongo wa nchini Afrika Kusini alisema ana maandalizi mazuri dhidi ya mpinzani wake ambaye anafahamu ana rekodi nzuri lakini ataingia ulingoni kwa ajili ya kuipambania Tanzania kiujumla kutafuta ushindi.
Promota wa pambano hilo kutoka PAF Promotion Company Ltd, Fadhili Maogola alisema: “Kutakuwa na mapambano takriban nane ya maandalizi kabla ya pambano la Mfaume na la mwisho la Kidunda, pia kutakuwa na burudani nyingi za kutosha kuelekea pambano hilo hivyo Watanzania wajitokeze kwa wingi siku hiyo wafurahi.”