Na mwandishi wetu
Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze amesema kwa sasa wanafanya kazi ya kupunguza presha ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa wachezaji wao ili watulize akili siku hiyo na kucheza kwa mipango waliyonayo.
Kaze amesema kila kitu kinakwenda sawa na wachezaji wako vizuri isipokuwa wameamua kushughulika na presha hiyo ili kuhakikisha wanapata matokeo stahiki kwenye mechi ya kwanza ya fainali hiyo.
Yanga itaumana na USM Alger ya Algeria katika fainali ya kwanza kihistoria kwa Yanga ya michuano hiyo keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kabla ya mechi ya marudiano Juni 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Julai 5, 1962, Algiers.
“Tunaendelea vizuri, wachezaji wote wako vizuri, kitu kizuri ni fainali ya Kombe la Afrika, ni mara ya kwanza kwenye historia kila mtu amehamasika, haina haja ya hamasa zaidi kwa wachezaji, wanafahamu ni pakubwa hapa tulipofika.
“Lakini nafikiri kilichopo sasa ni kushusha kidogo kwanza presha kwa wachezaji, wasiipeleke hiyo presha uwanjani, tunapaswa kujiandaa kwa mchezo, tucheze vile tunavyocheza huku tukifahamu tunatakiwa kufanya vizuri na kuongeza kitu kwa ajili ya mechi ya marudiano na tunaamini kila kitu kitakwenda sawa hiyo Jumapili,” alisema Kaze.
Kocha huyo pia aliwataka mashabiki wa soka na Watanzania kwa ujumla kwenda uwanjani kwa wingi ili kuitumia faida ya uwanja wa nyumbani ipasavyo kwa kuwapa sapoti wachezaji wa Yanga kwa dakika zote 90 huku wakiwabughudhi wapinzani kwa shangilia yao.









Naye kocha wa USMA, Abdelhak Benchikha ambaye ametua na kikosi chake usiku wa kuamkia jana amesema wamekuja kulitetea taifa la Algeria huku akitaka kuweka heshima kwa makocha wazawa kwa kutwaa kombe hilo.
“Tumekuja si kama klabu tu bali pia kama taifa la Algeria lakini pia kuwapa heshima makocha wazawa kama mimi baada ya kuifikisha timu hapa ilipo. Tunaifahamu Yanga, tunafahamu wametupeleleza nasi pia tumewapeleleza lakini dakika 90 uwanjani ndio zitaamua,” alisema Benchikha raia wa Algeria.