Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele amewashukuru mashabiki wa timu hiyo na Watanzania kwa kumpigia kura na kuwa mchezaji bora wa Afrika wa mwezi Aprili, mwaka huu.
Nyota huyo ametangazwa mchezaji bora jana Ijumaa usiku kupitia mchakato uliokuwa ukiendeshwa na mtandao maarufu wa soka Afrika, Foot Africa.
Katika kinyang’anyiro hicho Mayele amewazidi Msenegali, Ilman Ndiaye na Vincent Aboubakar raia wa Cameroon, wachezaji ambao alikuwa akichuanoa nao.
Mayele ameshinda kwa kura asilimia 32, Ndiaye anayekipiga Sheffield United ya England akiwa na asilimia 29 wakati Aboubakar anayeichezea Besiktas ya Uturuki akipata asilimia 16 ya kura 85,022 zilizopigwa.
Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Mayele aliandika ujumbe mfupi kuonesha kufurahia heshima hiyo na kuwashukuru Watanzania wote waliohusika katika ushindi wake huo.
“Asanteni sana Wananchi na Watanzania kwa ujulma kwa kura. Daima mbele nyuma mwiko,” alisema Mayele ambaye ni raia wa DR Congo.
Licha ya kuwa mpaka sasa ni kinara wa ufungaji katika Ligi Kuu NBC akiwa na mabao 16 na kuisaidia Yanga kukaribia kutetea ubingwa wake huo lakini katika mwezi Aprili pia aliisaidia Yanga kutinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza kwa kufunga mabao mawili pekee dhidi ya Rivers United ya Nigeria.
Mabao hayo yamemfanya Mayele kuwa kinara wa mabao wa michuano hiyo akifikisha mabao matano sawa na Ranga Chivaviro wa Marumo Gallants ya Afrika Kusini.
Mayele ambaye mpaka sasa amefunga mabao 30 kwenye michuano yote msimu huu, msimu uliopita alifunga mabao 16 kwenye ligi akimaliza nafasi ya pili nyuma ya George Mpole aliyefunga mabao 17 wakati akiitumikia Geita Gold.