London, England
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amepingana na hoja kwamba timu yake imeanza ‘kuchanganywa na presha’ za kulisaka taji la Ligi Kuu England (EPL) badala yake amewataka wachezaji kujenga moyo wa upambanaji.
Arsenal jana Jumapili ilijikuta ikiambulia sare ya mabao 2-2 na West Ham baada ya kutawala vyema mchezo na kuongoza kwa mabao 2-0 katika dakika 10 za mwanzo, mabao yaliyofungwa na Gabriel Jesus na Martin Odegaard.
West Ham walipata bao la kwanza dakika ya 33 lililofungwa na Saud Benrahma wakati dakika ya 40 Bukayo Saka akainyima Arsenal bao baada ya kukosa penalti na dakika tatu baadaye, West Ham wakapata bao la kusawazisha lililofungwa na Jarrod Bowen.
Japo bado Arsenal inaongoza ligi ikiwa mbele ya Man City inayoshika nafasi ya pili lakini tofauti ya pointi baina ya timu hizo inazidi kupungua.
Arsenal bado ipo kileleni kwa tofuati ya pointi nne dhidi ya Man City na siku 10 zijazo timu hizo zitakutana katika mechi inayotajwa kuwa muhimu kwa timu zote katika mbio za kulisaka taji la EPL.
Akiizungumzia sare na West Ham, Arteta alisema, “baada ya kuongoza 2-0 si kwamba tulikuwa na presha, hatukuuelewa mchezo, ni kwamba hatukuelewa mchezo ulichohitaji baada ya hapo.”
“Kwa mara nyingine tuliuanza mchezo vizuri mno, tulitawala mchezo, tulitawala uwanja na kufunga mabao mawili mazuri lakini baada ya hapo tukafanya kosa kubwa, tuliacha kucheza kwa malengo yale yale ya kutafuta goli la tatu na la nne,” alisema.
“Tukawa tu tunafikiria kwamba tunaweza kuwachezea na kubaki na matokeo hayo hayo, tuliona ni kitu rahisi na kwa wakati huo tukawapa matumaini, na kwa hilo tuwapongeze West Ham kwani waliiona nafasi hiyo,” alisema.