Na mwandishi wetu
Kikosi cha Simba leo Jumatano jioni kinatarajia kuingia kambini kuanza maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Yanga unaotarajia kupigwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Kuelekea katika mchezo huo, Kocha Mkuu wa Wekundu hao, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ameahidi ushindi katika pambano hilo licha ya kukiri kwamba ni mchezo mgumu kwao.
Akizungumza leo kocha huyo ambaye anacheza derby yake ya kwanza tangu atue Simba amesema kuwa kwao ni mchezo mkubwa ambao lengo namba moja ni kuchukua pointi zote tatu.
Alisema kutokana na hilo ndio maana walishaanza kuweka mikakati mapema ikiwemo kuwapumzisha baadhi ya wachezaji kwenye mchezo uliopita dhidi ya Ihefu.
“Siku nne zilizobaki zinatosha kujiandaa na mchezo huu ambao tumeupa uzito wa hali ya juu, kuna mazoezi maalumu kwa ajili ya mchezo huu, kitu kizuri kwetu wachezaji wote wapo katika hali nzuri akiwemo kipa Aishi Manula na beki Henock Inonga,” alisema Robertinho.
Robertinho alitamba kuwa katika rekodi zake za kucheza mechi za derby, hajawahi kufungwa tangu akiwa Uganda na Rwanda hivyo anataka kuiweka rekodi hiyo akiwa na kikosi cha Simba na anafurahi kwa sababu wapinzani wao Yanga wapo katika kiwango bora kwa sasa hivyo ni kipimo kizuri kwake.
Naye Meneja Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema wao kama viongozi wapo karibu na timu kuhakikisha wanashinda mchezo huo na kuwapa furaha mashabiki wao.
“Sisi kama menejimenti tunafanya kila kitu kwa upande wetu kuhakikisha tunapata ushindi, naamini hilo linasubiri muda tu kujitokeza, kitu cha msingi nawaomba mashabiki wetu waje kwa wingi uwanjani siku ya mchezo ili kuwapa sapoti wachezaji wao sababu huu ni mchezo wetu,” alisema Ally.