Na mwandishi wetu
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Pape Sakho ameitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Senegal kujiandaa na mchezo wa kufuzu fainali za Afcon 2023 dhidi ya Msumbiji.
Hiyo ni mara ya kwanza kwa mchezaji huyo kuitwa kwenye timu ya taifa tangu alipojiunga na miamba hiyo ya Tanzania mwanzoni mwa msimu uliopita akitokea Teungueth ya nyumbani kwao Senegal.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Senegal, vinaeleza kuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Aliou Cisse amemjumuisha Sakho baada ya kuvutiwa na kiwango chake anachokionesha akiwa na Simba kwenye michuano ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Ni mchezaji mwenye kipaji cha juu ukitaka kuthibitisha hilo msimu uliopita aliibuka mshindi wa bao bora kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, naamini anaweza kutusaidia kufikia malengo yetu dhidi ya Msumbuji,” alisema Cisse.
Katika orodha ya wachezaji 24, Sakho ataungana na baadhi ya nyota wengine wa timu hiyo wakiwemo mshambuliaji wa Bayern Munich, Sadio Mane, Gana Gueye anayekipiga Everton, Bamba Dieng anayecheza Lorient ya Ufaransa, Kalidou Coulibally wa Chelsea.
Sakho anaungana na wachezaji wengine wa Simba Henock Inonga (DR Congo), Clatous Chama (Zambia), Aishi Manula, Mzamiru Yassin, Beno Kakolanya ambao wameitwa kwenye timu zao za taifa kwa ajili ya kuwania kufuzu fainali za Afcon zinazotarajiwa kufanyika Ivory Coast.
Kimataifa Sakho aitwa timu ya Taifa Senegal
Sakho aitwa timu ya Taifa Senegal
Read also