Na mwandishi wetu
Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze amesema wapo tayari kupangwa na timu yoyote katika hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Azam Sports Federation (ASFC) au Kombe la FA, inayoendelea.
Yanga iliungana na Simba, Singida Big Stars na Geita Gold kutinga robo fainali baada ya kuilaza Prisons mabao 4-1 katika mchezo uliopigwa jana Ijumaa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Kocha huyo alisema kuwa juhudi na kujituma kwa wacheaji wao katika mchezo huo kumewapa matumaini ya kupata matokeo mazuri dhidi ya timu yoyote ambayo watapangiwa kwenye hatua hiyo.
“Tulicheza na timu ngumu inayocheza kwa kujilinda na kutumia nguvu nyingi lakini wachezaji wetu walijitahidi kupambana nao na kuonesha uwezo wao, kitu ambacho kimetupa ushindi na kutupeleka hatua inayofuata,” alisema Kaze.
Kaze ameeleza kuwa wataendelea kukiimarisha kikosi chao kwa kufanyia marekebisho mapungufu ambayo yamejitokeza kwenye mchezo huo ikiwemo mipira ya adhabu ndogo ambayo imekuwa ikiwaletea madhara siku za karibuni.
Naye kocha mkuu wa Prisons, Mohamed Abdallah ‘Bares’ amesema kadi nyekundu waliyoipata mwishoni mwa kipindi cha kwanza ndio imesababisha wapoteze mchezo huo kwa idadi kubwa ya mabao.
Bares alisema walikuwa bora kimbinu na kuwadhibiti washambuliaji wa Yanga, katika dakika 45 za kwanza lakini ubora na uzoefu waliokuwa nao wachezaji wa Yanga ilikuwa ni tatizo kwao na kujikuta wanapoteza mchezo.
“Nawapongeza Yanga na tunawatakia safari njema katika safari yao ya kutetea taji hilo lakini niseme kadi nyekundu ilituvurugia mpango wetu na kujikuta tunapoteza mchezo,” alisema Bares.