Na mwandishi wetu
Timu ya Yanga imeeleza kuwa imejipanga kesho Jumapili kurejesha furaha kwa mashabiki wake kwa kuibuka na ushindi watakapovaana na TP Mazembe ya Jamhuri ya Demokrasi ya Congo.
Yanga itaikaribisha Mazembe kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam katika mechi ya pili ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kwenye mchezo wa awali, Yanga ilipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya US Monastir ilipokuwa ugenini Tunis, Tunisia wakati Mazembe wakiibuka na ushindi wa mabao 3-1 ikiwa kwao dhidi ya Real Bamako ya Mali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi ameeleza kuwa wamejipanga kurudisha furaha ya mashabiki wao kwa kupata ushindi na kujiweka katika mazingira mazuri kwenye msimamo wa Kundi D ambalo linaongozwa na Mazembe.
“Utakuwa mchezo mgumu sana lakini nafurahi kuona wachezaji wameonesha ari kubwa ya ushindi kwenye uwanja wa mazoezi, kitu kizuri ni kwamba makosa ambayo yalisababisha tupoteze mechi yetu ya Tunisia tumeyafanyia kazi naamini hayatojirudia kwenye mchezo na Mazembe,” alisema Nabi.
Kocha huyo ameeleza kuwa katika mchezo huo atawakosa wachezaji watatu, Bernard Morrison ambaye bado anaendelea kuuguza majeraha ya nyonga, kiungo Salum Abubakary ‘Sure Boy’ anayeuguza mtoto wake na Stephane Aziz Ki ambaye ana asilimia ndogo za kucheza kutokana na kuchelewa kuripoti kambini baada ya mapumziko mafupi waliyopewa timu iliporejea nchini kutoka Tunisia.
Nabi pia alisema Yanga ina kundi kubwa la wachezaji hivyo anaamini wachezaji waliopo watapambana na kupata ushindi ambao ndio kusudio kubwa hiyo ni kutokana na kuwasoma vizuri wapinzani wao ikiwepo kuangalia mechi zao zilizopita za ligi na mashindano ya kimataifa.
Kocha Mkuu wa TP Mazembe, Mihayo Kazembe amesema wanatarajia kupata upinzani mkali kutoka kwa Yanga ambayo itakuwa na mchezaji wa 12 kutokana na kuwa uwanja wa nyumbani ila wamejipanga kukabiliana na hilo kuhakikisha hawapotezi mchezo.
“Mazembe ina bahati kubwa sana Tanzania, hatujawahi kufungwa hapa, mara zote tunapokuja hapa tunapata sare au ushindi, ninachoamini hata safari hii tutashinda ingawa najua mchezo utakuwa mgumu tena wenye ushindani mkubwa,” alisema Kazembe.
Kocha huyo amesema amekuja na kikosi chake kamili lengo ni kushinda mchezo huo ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo na anaamini vijana wake watatimiza vyema kile alichowaelekeza.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na matokeo mabaya waliyoyapata Yanga dhidi ya Monastir huku Mazembe iliyoanza kusukwa upya hivi karibuni ikihitaji kuendeleza rekodi yao Dar es Salaam na pia kuendelea kuongoza kundi hilo.