Doha, Qatar
Rais wa Fifa, Gianni Infantino amewatetea wenyeji wa fainali za Kombe la Dunia, Qatar na kuzishutumu nchi za Magharibi kwa unafiki kwa namna vyombo vya habari vya nchi hizo vinavyoripoti masuala ya haki za binadamu.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari alioufanya leo katika jiji la Doha, Infantino alizungumza kwa takriban saa moja na kuitetea Qatar pamoja na fainali za Kombe la Dunia ambazo zitaanza rasmi kesho Jumapili kwa wenyeji kucheza na Ecuador.
Kwa wiki kadhaa sasa kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia, vyombo vya habari vimekuwa vikitawaliwa na habari kuhusu rekodi mbovu za haki za binadamu za Qatar ikiwamo vifo vya wafanyakazi wahamiaji na namna ambavyo watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja wanavyonyimwa haki.
Infantino ambaye ni mzaliwa wa Switzerland mwenye uraia wa Italia, alisema kwamba mataifa ya Ulaya yanalazimika kuomba msamaha kwa matendo ya kihistoria yaliyofanywa na nchi hizo badala ya kuangalia suala la wafanyakazi wahamiaji wa Qatar.
Akifafanua zaidi Infantino alisema, “Leo nimeguswa mno katika fikra zangu, leo naifikiria Qatar, nawafikiria Waarabu, nawafikiria Waafrika, nawafikiria mashoga, nawafikiria walemavu, nawafikiria wafanyakazi wahamiaji.”
Moja ya taarifa kubwa ya gazeti moja la Uingereza iliyochapishwa mapema mwaka huu ilidai kwamba wafanyakazi wahamiaji zaidi ya 5,000 wamefariki wengi wao wakiwa kutoka nchi za Asia wakati wakishiriki kazi za ujenzi wa viwanja ingawa mamlaka za Qatar zimekana taarifa hiyo kwa madai kwamba si watu wote waliokufa chanzo chake ni ujenzi wa viwanja.
Infantino aliongeza, “mimi ni mtu wa Ulaya, kwa yale ambayo tumekuwa tukiyafanya kwa miaka 3,000 duniani kote tunalazimika kuomba msamaha kwa miaka 3,000 ijayo kabla ya kuanza kutoa somo la uadilifu kwa wengine.”
“Kama kweli Ulaya inajali thamani ya watu hawa, wanaweza kufuata mkondo wa kisheria, kama walivyofanya Qatar, hawa wafanyakazi wanaweza kuja Ulaya kufanya kazi, yaangalie mambo yao ya kesho, wapeni matumaini,” alisema.
“Napata ugumu kuzielewa shutuma hizi kwa Qatar, ni lazima tuwekeze katika kuwasaidia watu hawa kwenye elimu na kuwapa kesho yao iliyo bora na matumaini zaidi, ni lazima sote tujielemishe, mambo mengi hayajakamilika lakini mabadiliko na uboreshaji vinachukua muda,” alisema.
“Hili somo la uadilifu kwa upande mmoja ni unafiki tu, nashangaa kwanini hakuna hata mmoja anayetambua hatua nzuri iliyofikiwa hapa tangu mwaka 2016. Si rahisi kupokea shutuma zinazotokana na uamuzi uliofanywa miaka 12 iliyopita, Qatar ipo tayari na hizi zitakuwa fainali bora zaidi za Kombe la Dunia,” alisisitiza.
“Siitetei Qatar, watajitetea wenyewe mimi natetea soka, Qatar imepiga hatua na naona hivyo kwa mambo mengi pia, ni kweli kwamba mimi si raia wa Qatar au Muarabu au shoga, au mlemavu au mfanyakazi mhamiaji lakini najiwa na fikra kama wao, najua inamaanisha nini kwa kubaguliwa na kubughudhiwa ukiwa mgeni katika nchi ya kigeni.”
Kuhusu wafanyakazi wanaodaiwa kuumia na wengine kufariki, Infantino alisema kwamba kila mfanyakazi mwenye tukio la ajali ana malipo ya fidia kwa mujibu wa sheria kutegemena na aina ya tatizo, inaweza kuwa ni mishahara ya miaka kadhaa au namna nyingine.
Kuhusu marufuku ya bia kuuzwa kwenye viwanja vya soka ambayo imekuwa ikipigiwa kelele, Infantino alisema, “kama hili nalo ni jambo kubwa tulilonalo kwenye Kombe la Dunia basi itabidi nijiuzulu mara moja halafu niende zangu ufukweni nikajipumzikie.”
“Awali ya yote ngoja niwaambie kwamba kila uamuzi uliofikiwa hapa ni wa pamoja kati ya Fifa na wenyeji Qatar na kuhusu bia kuna maeneo mengi ya mashabiki kunywa bia, mashabiki watakunywa bia watakavyo, na nafikiri mtu asipokunywa bia kwa saa tatu bado ataendelea kuishi.”
“Sheria hizi hizi pia zinatumika Ufaransa, Hispania, Ureno na Scotland, hapa linakuwa jambo kubwa, au kwa sababu ni nchi ya kiislamu? Sijui ni kwa sababu gani.” alihoji Infantino.
Kimataifa Rais Fifa aitetea Qatar, alaumu unafiki
Rais Fifa aitetea Qatar, alaumu unafiki
Related posts
Read also