Na mwandishi wetu
Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mazingiza ameeleza kuwa hana mpango wa kuendelea kufanya kazi kwenye timu za Tanzania huku akisisitiza kuna mengi ya kufanya ili kulibadili soka la nchi hii ikiwamo kutenganisha siasa na mambo ya utawala.
Senzo ambaye ni raia wa Afrika Kusini ameeleza kuwa kila shirikisho na kila klabu linakuwa na mambo yake na kupitia Tanzania kuna mengi amejifunza ikiwemo mazingira kutomruhusu kufanya kazi kwa asilimia 100.
Ameeleza kwamba zaidi ya kuwa tayari Tanzania inapiga hatua kwenye soka lakini kama nchi inahitaji kubadilika na kupiga hatua zaidi kama itaweza kutenganisha siasa na utawala na kuacha weledi ufanye kazi yake.
“Unajua vitu katika weledi vinafanya kazi yake kwa njia ya tofauti na pia tunapaswa kujifunza kama unataka kuleta kitu kizuri unapaswa kujua ufanyeje, ni mazingira yanayohitaji umakini lakini unapaswa kuwa mkubwa, kuwa na moyo mkubwa, kutokuchukulia vitu kwa mazoea kwa ajili ya mustakabali wa klabu.
“Kuna kazi kubwa inapaswa kufanyika Tanzania kwa maana ya weledi, naweza kusema kuna kazi kubwa ya kufanya kutenganisha siasa na utawala na masuala ya media pia ingawa Tanzania inasogea lakini inatakiwa kuvitenganisha hivi vitu ili kazi ifanyike kweli na naamini soka la nchi hii litakuwa mara mbili zaidi ya hapa,” alisema Senzo.
Aidha, ofisa huyo alisema kuwa anajua watu wanajiuliza atakwenda wapi baada ya kuondoka Yanga lakini akasisitiza kuwa watulie, muda si mrefu itawekwa wazi na kubainisha kuwa hana mpango wa kufanya kazi Tanzania.
“Mimi ni mtu wa mpira tusubiri kuona nitaenda wapi lakini hakuna cha kuhofia, watatangaza wao watakaonichukua tusubiri ni watu wa mpira, ila siwezi kurudi |Tanzania, nitakuja kwa safari na mambo mengine lakini kufanya kazi Tanzania nafikiri nimeshafanya kwa sehemu yangu,” alifafanua Senzo.
Senzo alitua Tanzania kwa mara ya kwanza kama Mtendaji Mkuu wa Simba SC mwaka 2019 akichukua mikoba ya Crescentius Magori kabla ya kuihama klabu hiyo Agosti, 2020 na siku chache baadaye kutambulishwa kuiongoza Yanga kabla ya Julai 30, mwaka huu kutangazwa kuachia ngazi kwa Wanajangwani hao pia.
Soka Senzo: Klabu zitenganishe siasa, utawala
Senzo: Klabu zitenganishe siasa, utawala
Related posts
Read also