Na mwandishi wetu
Msemaji wa Yanga aliyefungiwa, Haji Manara amemuomba radhi Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa kwa kauli alizozitoa dhidi yake katika siku za karibuni.
Manara aliomba radhi hiyo akifafanua kuwa alifanya makosa kuikosoa kauli ya waziri huyo juu ya maadili na nidhamu aliyoitoa wakati wa hafla ya tuzo za Ligi Kuu Bara 2021/22 mnamo Julai 7, mwaka huu akihisi analengwa na kukosolewa yeye.
Manara alikosoa kauli za Mchengerwa wakati akieleza kutokubali kufungiwa na TFF kutojihusisha na soka ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha miaka miwili pamoja na faini ya Sh milioni 20 kwa kosa la kumtolea maneno yasiyofaa Rais wa TFF, Wallace Karia kwenye mechi ya fainali ya Kombe la FA iliyopigwa jijini Arusha.
“Kutokuelewa na ilichukuliwa hivyo na kwamba Waziri amemshukia Manara lakini na mimi vile vile kwa bahati mabaya niliingia kichwa kichwa, ilikuwa ndiyo wiki ile ile na hata katika ‘press’ yangu na wazee na baadhi ya viongozi waliingia hivyo pia kutokana na ile presha maana tukio lilitokea wiki ile ile tu.
“Na mimi katika maelezo yangu nikajikosea mimi, Serikali na waziri mwenyewe kuonyesha waziri alitoa malekezo kwa kiasi fulani, lakini baadaye nikafuatilia na kuzungumza na baadhi ya maofisa wa wizara wakanihakikishia kwamba hiyo ni ‘standard’ ameiweka waziri amekuwa anazungumzia maadili na nidhamu.
“Lilikuwa jambo jema analifanya waziri, yawezekana labda hawakuelewa tafsiri yangu ya lugha niliyotumia, kwa utashi wa kimaadili kama unasema jambo ambalo wenzio hawakuliona liko sahihi hakuna neno la kusema zaidi ya samahani, niseme samahani Waziri wangu, wizara na serikali yangu,” alisema Manara.
Manara pia alisema tayari wameshapokea barua ya hukumu na baada ya kupeleka malalamiko yao kwa mamlaka husika kuhusu kutosajiliwa kwa kanuni zilizotumika kumhukumu kupitia Kamati ya Maadili, sasa wiki hii yeye na mawakili wake wanajipanga kukata rufaa ya hukumu hiyo pia.
Soka Manara amuomba radhi Waziri
Manara amuomba radhi Waziri
Read also