Na mwandishi wetu
Klabu ya Simba imetangaza kuingia mkataba wa miaka mitano wenye thamani ya Sh bilioni 38 za Kitanzania na Kampuni ya Jayrutty Investment ambayo itahusika na mauzo ya jezi na mambo mengine.
Hafla ya kusaini mkataba huo ilifanyika Jumatano hii Aprili 16, 2025 na kuhudhuriwa na viongozi wa Simba na wadau mbalimbali wa michezo akiwamo naibu waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘MwanaFA’.
Menyekiti wa kamati ya tenda ya Simba, Seif Muba alisema kwamba walipokea barua nyingi za maombi ya tenda hiyo lakini ofa ya Jayrutty imewashawishi kuwapa tenda hiyo.
Muba alisema kwa mantiki hiyo wamekubali kuwapa Jayrutty haki ya matumizi ya nembo ya klabu ya Simba kwa vile mbali na fedha kuna manufaa mengine mengi kwa klabu yao.
Alisema awali kampuni nane zilijitokeza lakini ni sita ndizo zilizowasilisha madokezo yao na kila kitu kilikuwa wazi kabla ya Jayrutty kushinda tenda hiyo na tayari wameweka kiasi cha Sh bilioni 38.
Akizungumzia mkataba huo, Mkurugenzi wa Jayrutty Investment, Joseph Rwagasira alizitaja baadhi ya faida ambazo klabu ya Simba itazipata kupitia mkataba huo kwa kipindi chote cha miaka mitano.
Rwegasira alisema jambo la kwanza watakalofanya ni kuijengea klabu hiyo uwanja wenye uwezo wa kuchukua mashabiki kati ya 10,000 hadi 12,000 na watafanya hivyo katika uwanja wa klabu hiyo uliopo Bunju, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Alisema kwamba mbali na ujenzi huo lakini pia kila mwaka watatoa Sh milioni 100 kwa ajili ya soka la vijana, sh milioni 100 nyingine kwa maandalizi ya msimu na kiasi kingine kama hicho kwa ajili ya tamasha la Simba Day.
Sambamba na hilo, Jayrutty pia watatoa Sh milioni 450 kwa kila mwaka fedha ambazo zitakwenda kwa wachezaji wakati jezi za klabu hiyo sasa zitatengenezwa na kampuni kubwa duniani ingawa hakuitaja jina.
Kwa upande wake naibu waziri Mwana FA alisema serikali inapongeza kuingia kwa mkataba huo huku akielezea kuvutiwa zaidi na mpango wa ujenzi wa uwanja.
Mwana FA alisema uwanja huo unaweza kutumiwa kwa mechi za ndani wakati zile za kimataifa zikiendelea kuchezwa kwenye Uwanja wa Mkapa ambao pia utakuwa umepunguziwa matumizi.
Kimataifa Simba yaingia mkataba wa bilioni 38
Simba yaingia mkataba wa bilioni 38
Read also