Na mwandishi wetu
Yanga imetua kibabe hatua ya nusu fainali Kombe la Shirikisho CRDB kwa kuilaza Stand Utd mabao 8-1, mechi iliyochezwa leo Jumanne Aprili 15, 2025 kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
Bao la kwanza la Yanga lilipatikana dakika ya 15 mfungaji akiwa Stephanie Aziz Ki aliyefunga kwa guu la kulia akiitumia pasi ndefu ya Maxi Nzengeli na kumpiga chenga kipa Amir Mashenji.
Yanga iliandika bao la pili dakiika saba baadaye mfungaji akiwa ni beki wa kushoto, Nickson Kibabage ambaye aliitumia pasi ndefu ya Aziz Ki.
Bao la tatu la Yanga lilifungwa na Clatous Chama dakika ya 32, bao lililotokana na pasi ya Chama kwa Aziz Ki ambaye alimrudishia mpira Chama ambaye alimpiga chenga beki kabla ya kuujaza mpira wavuni.
Zikiwa zimebakia dakika tano timu kwenda mapumziko Yanga waliandika bao la nne mfungaji akiwa Chama kwa mara nyingine baada ya Aziz Ki kumpigia pasi ndefu na mpira kuwagonga mabeki wa Stand kabla ya kumkuta mfungaji.
Dakika moja kabla ya timu kwenda mapumziko, Stand walionesha uhai na kufanya shambulizi lililoanzia nyuma kabla ya mpira kumkuta Kigi Makasy lakini shuti lake la mguu wa kushoto lilipaa juu ya goli.
Kipindi cha pili, Stand waliendeleza moto wao na hatimaye kupata bao pekee dakika ya 49 lililofungwa na Msenda Senda ambaye aliingia uwanjani kuchukua nafasi ya Kigi.
Senda alionesha uwezo binafsi hadi kufunga bao hilo baada ya kuambaa na mpira kabla ya kumlamba chenga beki wa Yanga, Bakari Mwamnyeto na kufumua shuti lililomshinda kipa Djigui Diarra.
Bao hilo ni kama liliwatia hasira Yanga ambao waliongeza bao la tano dakika ya 51 likifungwa tena na Aziz Ki kwa mpira wa adhabu iliyotolewa baada ya Jonathan Ikangalombo kuchezewa rafu.

Dakika ya 60 Aziz Ki tena aliifungia Yanga bao la sita na la tatu (hat trick) kwake akiutumia mpira ulioanzia kwa Ikangalombo aliyempasia Chama ambaye naye alimpasia mfungaji na kuujaza mpira wavuni.
Aziz Ki ambaye aliibuka mchezaji bora wa mechi hiyo ni kama vile hakutosheka na hat trick baada ya kuifungia Yanga bao la saba na la nne kwake, safari hii akifunga kwa shuti la mbali.
Yanga walikamilisha karamu ya mabao kwa bao la nane lililofungwa na Kennedy Musonda ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Prince Dube, Musonda alifunga bao hilo kwa pasi ya Farid Mussa ambaye naye aliingia badala ya Aziz Ki.
Yanga sasa inasubiri kuumana na JKT Tanzania katika nusu fainali ya michuano hiyo inayodhaminiwa na Benki ya CRDB wakati mahasimu wao Simba wataumana na Singida Black Stars katika nusu fainali ya pili, mechi ambazo washindi wake watacheza mechi ya fainali.