Miami, Marekani
Rais wa Shirkisho la Soka Marekani Kaskazini, Kati na Carribean (Concacaf), Victor Montagliani amepinga wazo la kiongozi wa Shirikisho la Soka Marekani Kusini (CONMEBOL), Alejandro Domínguez kutaka timu shiriki kwenye fainali za Kombe la Dunia 2030 ziwe 64.
Domínguez aliwasilisha rasmi wazo la kupanua mashindano hayo kwenye kikao cha Baraza la Fifa kilichoendeshwa kwa mtandao akisisitiza timu shiriki ziongezwe kutoka 32 za sasa hadi kufikia 64.
“Kwa upande wetu Concacaf, tumeonesha tupo wazi kwa mabadiliko kwa kuunga mkono fainali za Kombe la Dunia kwa wanawake pamoja na muendelezo wa mabadiliko wa mashirikisho yetu kwa timu za wanaume na wanawake na mashindano ya klabu,” alisema Montagliani.
“Sidhani kama kuongeza timu katika fainali za Kombe la Dunia za wanaume kufikia 64 ni hatua sahihi kwa mashindano hayo pamoja na mustakabali mpana wa soka kwa mashindano ya timu za taifa, klabu, ligi na wachezaji,” alisema Montagliani.
Fifa itaanza kufanya majaribio ya mfumo wa timu 48 kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026 lakini Domínguez alisisitiza haja ya kufanya zaidi ya hilo kwa kupanua wigo wa mashindano.
Naye Rais wa Umoja wa Vyama vya Soka Ulaya (Uefa) Aleksander Čeferin pia alionesha kutounga mkono hoja ya Domínguez akisema wazo la kuongeza idadi ya timu ni baya.
“Nafikiri ni wazo baya, si wazo zuri kwa fainali zenyewe za Kombe la Dunia, na pia si wazo zuri kwa timu zinazofuzu, kwa hiyo siungi mkono wazo hili, sijui limetokea wapi lakini ni hatari kwa sababu hatukufahamu lolote kabla ya wazo hili katika Baraza la Fifa,” alisema Ceferin.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Soka Asia, (AFC), Sheikh Salman bin Ibrahim alisisitiza kwamba ongezeko la idadi hiyo litahamasisha na kuwa mwanzo wa mvurugano.
“Kama jambo hili litakuwa wazi kwa mabadiliko maana yake ni kwamba mlango utakuwa wazi kwa kuongeza timu 64 lakini kuna mtu pia anaweza kuja na hoja ya kutaka idadi ya timu ifikie 132, mwisho itakuwaje? Ni mvurugano,” alisema Sheikh Salman.
Katika fainali za Kombe la Dunia 2026, majaribio yatafanyika kwa timu 48 ikiwa ni kwa mara ya kwanza katika historia ya fainali hizo zitakazochezwa Marekani, Mexico na Canada.