Istanbul, Uturuki
Kocha wa klabu ya Fenerbahce ya Uturuki, Jose Mourinho amefungiwa mechi tatu pamoja na kupigwa faini ya dola 7.735 baada ya kumminya pua kocha wa Galatasaray, Okan Buruk.
Uamuzi huo umefikiwa na Shirikisho la Soka Uturuki (TFF) baada ya kujiridhisha na kosa hilo ambalo Mourinho anadaiwa kulifanya wakati wa mechi ya timu hizo mahasimu yaani Istanbul Derby.
Mourinho, 62, anadaiwa kufanya kitendo hicho Jumatano katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Uturuki iliyoisha kwa Fernerbahce anayoinoa Mourinho na iliyokuwa uwanja wa nyumbani kulala kwa mabao 2-1.
Hali ya tafrani iliibuka katika mechi hiyo baina ya wachezaji hadi mwamuzi kulazimika kuwapa kadi nyekundu wachezaji watatu, wawili wakiwa wa Galatasaray.
Baada ya mwamuzi kupuliza filimbi ya kumaliza mechi, Mourinho alionekana akimminya Buruk puani ambapo kocha huyo alianguka chini katika namna ambayo kwa tafsiri ya wengi ilikuwa kama kulikuza zaidi tukio hilo.
“Mourinho amelazimika kufungiwa kuingia katika vyumba vya kubadilishia nguo na kwenye benchi kwa mechi tatu zilizo rasmi,” ilieleza taarifa ya TFF.
Kwa mantiki hiyo Mourinho ambaye timu yake inashika nafasi ya pili katika ligi ikiwa imetanguliwa na mahasimu wao, Galatasaray kwa tofauti ya pointi sita, atazikosa mechi dhidi ya Kayserispor, Trabzonspor na Sivasspor.