Na mwandishi wetu
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeufungulia Uwanja wa Liti mjini Singida baada ya kufanya maboresho yaliyokidhi vigezo vilivyosababisha kufungiwa kwa uwanja huo.
Taarifa ya TFF iliyopatikana leo Jumanne na kusainiwa na Ofisa Habari na Mawasiliano wa shirikisho hilo, Clifford Ndimbo (pichani) ilizitaja sababu za kufungiwa uwanja huo kuwa ni miondombinu yake kutofaa.
Uwanja huo kwa mujibu wa TFF umekaguliwa na kuonekana umekidhi vigezo vya kikanuni baada ya marekebisho yanayodaiwa kufanywa na wamiliki wa uwanja huo.
TFF imeendelea kuzikumbusha klabu kwa kushirikiana na wamiliki wa viwanja hivyo kuhakikisha wanaboresha na kutunza miundombinu yake ili viweze kutumika kwa mechi za ligi.
Kwa mujibu wa taarifa ya TFF uboreshaji wa viwanja unasaidia kuongeza ushindani pamoja na thamani ya ligi.
Katika siku za hivi karibuni, TFF imekuwa ikivifungia viwanja kadhaa kutokana na mapungufu mbalimbali kwa kutokidhi vigezo vya kikanuni na sheria za mpira wa miguu.
Miongoni mwa viwanja vilivyofungiwa na TFF ni ule wa Jamhuri mjini Dodoma ambao pia umeshafunguliwa baada ya kufanya maboresho yaliyozingatia kanuni na sheria za mchezo wa soka.
Soka TFF yaruhusu Uwanja Liti kutumika
TFF yaruhusu Uwanja Liti kutumika
Read also