Manchester, England
Kocha wa Man City, Pep Guardiola ametoa kauli ya kujishusha na kujitoa katika kuliwania taji la Ligi Kuu England (EPL) akidai kwamba kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya yatakuwa mafanikio makubwa kwa timu yake msimu huu.
Man City ambao wamekuwa mabingwa wa EPL kwa miaka minne iliyopita kwa sasa wanashika nafasi ya tano katika ligi hiyo iliyobakiza mechi 10 huku kikosi chao kikikabiliwa na janga la wachezaji majeruhi.
Mmoja wa wachezaji ambaye amekuwa majeruhi tangu Septemba mwaka jana ni Rodri, nyota wa timu hiyo ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or.
Pep anaamini kutokana na mambo anayokabiliana nayo katika kikosi chake, kufuzu nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya yatakuwa mafanikio ya maana kwa timu hiyo.
“Kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya yatakuwa mafanikio makubwa lakini lazima tuwe wenye kupata ushindi, nataka tufuzu, halitokuwa jambo zuri kama City watakosekana kwenye michuano hiyo,” alisema Pep.
Akifafanua kuhusu hilo, Pep alisema kuzikosa fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya ni tatizo ingawa alkiri kuna timu zilizoshindwa kufuzu lakini kwa sasa zimo kwenye michuano hiyo.
Man City hata hivyo wanaweza kufuzu fainali hizo wakiwa nafasi ya tano kutokana na ubora na mafanikio ya timu za England kwenye michuano ya Uefa na hivyo kuifanya EPL kuwa na timu tano kwenye ligi hiyo.
Hali ikiwa hivyo itakuwa salama kwa Man City ingawa Pep alisema haangalii hilo badala yake anataka timu yake iwe yenye kupata ushindi kuanzia sasa hadi mwisho wa msimu kwani katika michezo kuna nafasi za tano au sita au saba na zote hizo kuzipata lazima uwe mwenye kushinda mechi zako.