Istanbul, Uturuki
Mshambuliaji wa zamani wa Chelsea, Didier Drogba amemtetea aliyekwua kocha wake katika timu hiyo, Jose Mourinho akisema kwamba kocha huyo si mbaguzi wa rangi.
Klabu ya Galatasaray ya Uturuki imemtuhumu Mourinho ambaye kwa sasa anainoa Fenerbahce kwa kutoa kauli ya kibaguzi baada ya timu hizo mahasimu kutoka sare ya bila kufungana juzi Jumatatu.
Akizungumza baada ya mechi hiyo maarufu Istanbul Derby, Mourinho alisema kwamba benchi la timu pinzani ambao ndio wenyeji wa mechi hiyo walikuwa wakiruka kama nyani.
Drogba (pichani chini) amewahi pia kuichezea Galatasaray katika msimu wa 2013-14 na kuifungia mabao 20 katika mechi 53, hakubaliani na tuhuma hizo na ameamua kumtetea bosi wake huyo wa zamani.
“Mnajua jinsi nilivyojivunia kuvaa jezi ya njano na nyekundu na mapenzi yangu kwa klabu yenye hadhi nchini Uturuki, sote tunajua jinsi hamasa na uhasama vinavyoweza kuwa na mimi ni mwenye bahati kukutana na mambo haya,” alisema Drogba.
“Nimesikia maoni ya hivi karibuni kuhusu Jose Mourinho, niamini mimi ninapokwambia namjua Jose kwa miaka 25 na si mbaguzi na historia ya siku za nyuma na ya sasa ipo kuthibitisha hilo, ‘baba’ yangu anawezaje kuwa mbaguzi, hapana jamani,” alisema Drogba.
Mourinho ambaye mbali na Chelsea pia amewahi kuzinoa Man United, Real Madrid, FC Porto na Inter Milan, alianza kibarua cha kuinoa Fenerbahce Juni mwaka jana baada ya kuachana na Roma ya Italia.

Mourinho aliwahi kutoa shutuma kwa waamuzi wa Uturuki akisema kwamba ingekuwa majanga kuwatumia waamuzi hao.
Mechi ya Fanarbahce na Galatasaray ilichezeshwa na mwamuzi Slavko Vincic ambaye anatokea nchini Slovenia baada ya timu zote kuomba mwamuzi kutoka nje ya Uturuki achezeshe mechi hiyo.
Inadaiwa Mourinho amekerwa na tuhuma hizo na anaangalia uwezekano wa kuchukua hatua za kisheria, amefanya kazi na wachezaji wengi weusi wenye asili ya Afrika na inaaminika hakuna anayeweza kuamini kocha huyo kujihusisha na ubaguzi wa rangi.