Madrid, Hispania
Mchezaji wa timu ya taifa ya wanawake ya Hispania, Jenni Hermoso aliyepigwa busu la mdomoni amesema adhabu iliyotolewa kwa Luis Rubiales aliyempiga busu ibaki kuwa somo.
Wakati wa utoaji tuzo kwa timu ya wanawake ya Hispania, Jenni alipigwa busu la mdomoni na Rubiales wakati huo akiwa rais wa Shirikisho la Soka Hispania, tukio ambalo lilizua mjadala mkubwa duniani kote.
Hivi karibuni Mahakama Kuu Hispania ilimpa Rubiales adhabu ya faini ya Dola 10,700 kwa kosa la udhalilishaji kijinsia pamoja na marufuku ya kumsogelea Jenni kwa umbali usiozidi mita 200 na kutofanya mazungumzo naye kwa mwaka mmoja.
Rubiales, 47, ambaye alilazimika kujiuzulu nafasi ya urais wa Shirikisho la Soka Hispania, hata hivyo alifutiwa tuhuma za kutumia nguvu na kumlazimisha Jenni aseme kwamba busu hilo alipigwa kwa makubaliano.
Akizungumzia sakata hilo na uamuzi wa mahakama kwa mara ya kwanza, Jenni alitumia mtandao wa Instagram na kusisitiza kwamba uamuzi wa mahakama ni hatua muhimu.
Jenni hata hivyo aliongeza kwa kusema kwamba kwa mazingira yanayowazunguka katika jamii bado kuna mengi yanatakiwa kufanywa.
“Moyo wangu upo kamili pamoja na kila mtu ambaye amekuwa na ataendelea kuwa pamoja nami katika mapambano haya, na sasa yamefikia mwisho,” alisema Jenni.
Ijumaa iliyopita, Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) iliitupa rufaa iliyowasilishwa na Rubiales ya kupinga adhabu ya kufungiwa kujihusisha na soka kwa miaka mitatu aliyopewa na Fifa.