Na mwandishi wetu
Yanga imeendeleza makali katika Ligi Kuu NBC ikijiimarisha kileleni kwa kuipiga Mashujaa FC mabao 5-0 au mkono, mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, leo Jumapili, Februari 23, 2025.
Katika mechi hiyo wenyeji Mashujaa walionesha uhai kuanzia kipindi cha kwanza kwa kuwadhibiti Yanga kabla ya mambo kuwaharibikia dakika ya 33 baada ya Duke Abuya kuifungia Yanga bao la kwanza.
Bao hilo lilidumu kipindi chote cha kwanza kabla ya Yanga kuandika bao la pili dakika tatu baada ya kuanza kipindi cha pili, bao lililofungwa kwa kichwa na Prince Dube akiitumia pasi ya Pacome Zouzoua.
Bao hilo limempaisha Dube na kuungana na wachezaji wengine wawili wenye mabao 10 katika ligi hiyo ambao ni mshambuliaji mwenzake wa Yanga, Clement Mzize na kiungo wa Simba Jean Ahoua.
Yanga waliandika bao la tatu dakika ya 55 lililofungwa na Khalid Aucho ambaye kama ilivyokuwa kwa Dube naye alineemeka na pasi ya Pacome ambaye pia aliibuka mchezaji bora wa mechi hiyo.
Mabao mengine ya Yanga yalifungwa na Clatous Chama aliyeingia uwanjani dakika ya 68 akichukua nafasi ya Stephane Aziz Ki, Chama alifunga mabao hayo dakika za 74 na 83.
Kwa ushindi huo Yanga imefikisha pointi 55 katika michezo 21 ikifuatiwa na mahasimu wao Simba wanaoshika nafasi ya pili wakiwa na pointi 50 baada ya kucheza mechi 19.
Soka Yanga yaipiga mkono Mashujaa
Yanga yaipiga mkono Mashujaa
Read also