London, England
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amewalaumu wachezaji wake kwa kutocheza katika kiwango cha kuwapa ushindi katika mechi ya jana Jumamosi dhidi ya West Ham ambayo walilala kwa bao 1-0.
Bao pekee la Jarrod Bowen dakika ya 44 lilitosha kuifanya West Ham iliyokuwa ugenini kutoka na ushindi huku Arteta akilalamikia kiwango cha timu yake iliyoambulia mashuti mawili tu ya maana langoni mwa wapinzani wao.
Matokeo hayo yanairudisha nyuma Arsenal katika mbio za kuishusha Liverpool kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England (EPL) ikiwa nafasi ya pili na sasa imezidiwa na Liverpool kwa tofauti ya pointi nane.
Liverpool inaweza kuongeza tofauti hiyo ya pointi na kuwa kubwa zaidi iwapo itashinda mechi yao ya leo Jumapili dhidi ya mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Man City.
Kutokana na janga la wachezaji majeruhi, Arsenal jana ilicheza bila ya Kai Havertz, Gabrieli Martinelli, Gabrieli Jesus na Bukayo Saka hivyo timu kutokuwa na mshambuliaji tegemeo badala yake kiungo Mikel Merino akabeba jukumu hilo.
Alipoulizwa kama kukosekana mshambuliaji mwenye sifa na tegemeo kama ndiko kulikoikwaza Arsenal, Arteta alipingama vikali na mtazamo huo.
“Hapana, hapana nalikataa hilo moja kwa moja kwa sababu hapa nazungumzia kiwango cha wachezaji na timu ambayo tumecheza nayo nikiwamo mimi,” alisema Arteta.
Arteta pia alisema kwamba ingawa timu yake ilijitahidi kumiliki mpira na kupiga mashuti lakini hakuona kama ilikuwa katika kiwango kilichohitajika hasa kwa kuwa walipoteza mipira mingi na kuwapa nafasi wapinzani wao kuwakimbiza.