Madrid, Hispania
Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Hispania, Luis Rubiales amekutwa na hatia katika kesi ya udhalilishaji kijinsia baada ya kumpiga busu la mdomoni mchezaji wa timu ya wanawake ya Hispania, Jenni Hermoso.
Rubiales alimpiga mchezaji huyo busu lililozua taharuki wakati wa utoaji tuzo mara baada ya Hispania kuibuka mshindi wa fainali za Kombe la Dunia la Wanawake mwaka 2023.
Mahakama Kuu Hispania baada ya kumkuta na hatia katika kosa hilo imetaja adhabu ya faini ya Dola 10,400 kwa kosa hilo lakini imemfutia kosa la kutoa vitisho au ubabe.
Rubiales mara baada ya kutajiwa hukumu hiyo alisema kwamba anajipanga kukata rufaa akiahidi kuendeleza mapambano.
Awali waendesha mashtaka walitaka Rubiales afungwe jela kwa tukio hilo ambalo liliibua mijadala ya udhalilishaji jinsia na haki za wanawake ingawa mwenyewe alidai kwamba Jenni alikubali kupigwa busu.
Jaji mmoja wa mahakama hiyo alisema anauamini ushahidi uliotolewa na Jenni kwa kudai kwamba hakukuwa na makubaliano kati yake na Rubiales kwenye tukio zima la kupigwa busu mdomoni.
Jaji huyo hata hivyo alipinga suala la ubabe au vitisho vya aina yoyote kutumika katika tukio hilo na hivyo hakuona uhalali wowote wa kumpa Rubiales adhabu ya kifungo cha jela.
Rubiales pia ametakiwa kutomsegelea Jenni kwa umbali wa mita 200, pamoja na kutozungumza naye kwa mwaka mmoja.

Wakati kesi ikiendelea, Jenni alisema busu alilopigwa bila ridhaa yake lilimfanya akose raha katika siku ambayo ilikuwa ya furaha ya maisha yake wakati wachezaji wenzake walisema kwamba mwenzao alilia na kujiona mnyonge kwa saa na siku kadhaa.
Katika hatua nyingine Watuhumiwa wengine watatu waliodaiwa kuhusika kwa kutoa vitisho na ushawishi ili suala hilo lisifike mbali wote wamefutiwa mashtaka na kuachiwa huru.
Watuhumiwa hao ni aliyekuwa kocha timu ya wanawake ya Hispania, Jorge Vilda, mkurugenzi wa michezo wa timu ya soka ya wanaume ya Hispania, Albert Luque na mkurugenzi wa masoko wa Shirikisho la Soka Hispania, Ruben Rivera.
Baada ya hukumu kutolewa Chama cha Wanasoka Hispania (AFE) kimesema kwamba hukumu hiyo ni hatua muhimu katika kulinda haki za wanawake na kupigania michezo ambayo haitokuwa na unyanyasaji na ubaguzi.