Madrid, Hispania
Aliyekuwa rais wa Shirikisho la Soka Hispania, Luis Rubiales ameiambia mahakama moja ya Hispania kuwa alimuomba kumpiga busu mchezaji wa timu ya taifa ya Hispania, Jenni Hermoso kabla ya kufanya tendo hilo.
Rubiales aliingia matatani kwa kumpiga busu mdomoni Jenni katika shamrashamra za kutoa tuzo kwa wachezaji wa timu ya taifa ya wanawake ya Hispania iliyobeba Kombe la Dunia mwaka 2023.
Sakata hilo lilikuwa mahakamani leo Jumanne ambapo mbali na Rubiales, viongozi wengine watatu wanatuhumiwa kwa kosa la kutaka busu ambalo Rubiales alimpiga Jenni lionekane ni tukio la kawaida na kupuuzwa.
Katika sakata hilo, Rubiales pia anatuhumiwa kwa udhalilishaji wa kijinsia pamoja na wenzake watatu wanaodaiwa kumshawishi, Jenni amtetee Rubiales.
Watuhumiwa hao watatu ni kocha wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake Hispania, Jorge Vilda, mkurugenzi wa zamani wa michezo wa timu ya taifa ya wanaume ya Hispania, Albert Luque na mkurugenzi wa masoko wa Shirikisho la Soka Hispania, Ruben Rivera.
“Nina hakika alinipa ruhusa, kwa wakati ule lilikuwa jambo ambalo ni la kawaida,” alisema Rubiales kuiambia mahakama.
Alipoulizwa kama ana kawaida ya kuwabusu watu kwenye midomo, Rubiales alisema kwamba kwa tukio lilivyokuwa na kutokana na ukweli kwamba amekuwa akimjua Jenni kwa muda mrefu ilimhalalishia kufanya alichokifanya.
Rubiales pia alifafanua kwamba Kombe la Dunia huwa hawashindi kila siku na angeweza kufanya hivyo hata kwa mchezaji wa kiume au hata kwa mmoja wa watoto wake.
Kwa upande wake Jenni alisema hakutoa ruhusa kwa Rubiales kumpiga busu mdomoni wakati Rubiales amekana kufanya kosa lolote na kusisitiza kwamba alichokifanya kilikuwa na ridhaa ya Jenni.
Baada ya tukio la busu hilo, Rubiales alijikuta akisakamwa hadi akalazimika kujiuzulu nafasi ya urais kwenye shirikisho la soka na kufungiwa na Fifa kwa miaka mitatu.
Katika hoja zake za awali, Jenni alisema baada ya kupigwa busu alijiona aliyedharauliwa na kwamba busu hilo lilimtoa katika tukio la furaha ya maisha yake baada ya Hispania kushinda Kombe la Dunia.
Waendesha mashtaka katika shauri hilo wanataka Rubiales afungwe jela kwa miaka miwili na nusu na kutozwa faini ya Dola 51,000 pamoja na kupigwa marufusu kujihusisha na shughuli za michezo.
Kuhusu watuhumiwa wengine watatu, waendesha mashtaka hao wanataka wafungwe jela kwa mwaka mmoja na nusu kwa kila mmoja.
Kimataifa Aliyempiga busu mchezaji adai aliomba kabla
Aliyempiga busu mchezaji adai aliomba kabla
Read also