Na mwandishi wetu
Yanga imerejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu NBC kwa kishindo baada ya kuikandika Ken Gold FC mabao 6-1 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa KMC, Kinondoni, Dar es Salaam, leo Jumatano, Februari 5, 2025.
Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi 45 katika mechi 17 wakifuatiwa na mahasimu wao Simba waliokuwa wakishika usukani kabla ya mechi ya leo ambao sasa wameshuka hadi nafasi ya pili wakiwa na pointi 43 katika mechi 16.
Mashujaa wa Yanga walikuwa ni Prince Dube na Clement Mzize ambao kila mmoja alifunga mabao mawili na mengine yakifungwa na Pacome Zouzoua na Duke Abuya wakati bao pekee la Ken Gold lilifungwa na Seleman Rashid.
Karamu ya mabao ya Yanga ilianzia dakika ya pili kwa bao la Dube baada ya kuinasa pasi ya Stephane Aziz Ki na dakika nne baadaye waliongeza bao la pili lililofungwa na Mzize.
Mabao mengine mawili ya Yanga yalifungwa na Pacome dakika ya 35 na Mzize tena dakika ya 44 na kuiwezesha Yanga kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 4-0.
Kipindi cha pili Yanga ilikianza kwa kasi na kuandika bao la tano lililofungwa na Dube dakika ya 47 wakati karamu hiyo ilihitimishwa na Abuya aliyefunga bao la sita katika dakika ya 85.
Dakika moja baada ya Abuya kufunga bao hilo, Ken Gold walifurukuta na kupata bao pekee la kufutia machozi lililofungwa na Seleman Rashid aliyefumua shuti kali na kumshinda kipa Djigui Diara.
Matokeo hayo yanazidi kuwaweka pabaya Ken Gold ambao hadi sasa wanaburuza mkia wakiwa na pointi sita tu katika mechi 17 walizocheza.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa mapema leo, Tabora United ikiwa nyumbani iliichapa Namungo FC mabao 2-1.
Kimataifa Yanga yarejea kileleni kwa kishindo
Yanga yarejea kileleni kwa kishindo
Read also