Rio de Janeiro, Brazil
Klabu ya Santos ya Brazil ipo katika mazungumzo kumsajili mshambuliaji wake wa zamani, Neymar Jr ambaye mkataba wake wa sasa na klabu ya Al Hilal ya Saudi Arabia umesitishwa kwa makubaliano ya pande mbili.
Neymar, 32, ambaye pia ni mshambvuliaji wa timu ya taifa ya Brazil, anatarajia kusaini mkataba mfupi na klabu yake hiyo ya zamani iliyomsaidia kukuza kipaji chake cha soka.
Usajili wa Neymar katika klabu ya Al Hilal uliofanyika Agosti 2023, ulikuwa tukio kubwa katika soka ukigharimu Pauni 77.7 milioni lakini mchezaji huyo aliishia kuichezea timu hiyo mara saba tu kabla ya kuanza kuandamwa na majeraha.
Katika msimu huu, Neymar aliichezea timu hiyo mara mbili tu na zote aliingia akitokea benchi hali ambayo kwa kiasi kikubwa imechangiwa na tatizo la kuwa majeruhi.
“Klabu ya Al Hilal inamshukuru na kuthamini alichokifanya Neymar kwa kipindi chote na kumtakia mafanikio katika maisha yake ya soka,” ilieleza taarifa ya Al Hilal.
Klabu nyingine iliyoonesha nia ya kutaka kumsajili Neymar ni Chicago Fire ya Marekani lakini mchezaji huyo alionekana kuvutiwa zaidi na mpango wa kurudi kwao Brazil katika klabu ya Santos.
Pia zipo habari kwamba klabu nyingine ya Marekani, Inter Miami nayo imekuwa ikimpigia hesabu Neymar na kama hilo lingefanikiwa mchezaji huyo angeungana na nyota mwenzake wa zamani wa Barca, Lionel Messi ambaye anaichezea timu hiyo.
Mkataba wa Neymar na Al Hilal unafikia tamati miezi takriban saba ijayo baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili na mshahara unaofikia Pauni 129 milioni kwa mwaka.
Kwa sasa Neymar anabaki kuwa mchezaji ghali zaidi duniani tangu ajiunge na PSG mwaka 2017 kwa ada ya Pauni milioni 200.