Na mwandishi wetu
Safari ya Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika imefikia tamati leo Jumamosi ya Januari 18, 2024 baada ya kutoka sare ya bila kufungana na MC Alger ya Algeria kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga kumaliza nafasi ya tatu katika Kundi A ikiwa na pointi nane wakati Alger imefikisha pointi tisa na kushika nafasi ya pili nyuma ya Al Hilal ya Sudan.
Timu nyingine katika kundi hilo ni TP Mazembe ya DR Congo ambayo imemaliza mechi zake hii leo ikiwa mkiani wakati Al Hilal na MC Alger zikisonga mbele hatua ya robo fainali.
Wenyeji Yanga waliuanza mchezo kwa dhamira ya kusaka ushindi na haikushangaza kuutawala mchezo kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha kwanza kwa kulisakama lango la Alger lakini tatizo likawa kwenye umaliziaji.
Stephane Aziz Ki alianza kuonesha makali yake mapema dakika ya 11 baada ya kuambaa na mpira upande wa kushoto wa Alger na kuwazidi ujanja walinzi wa Alger kabla ya kufumua shuti lililookolewa na kipa.
Clement Mzize naye alipata nafasi mbili lakini alishindwa kuzitumia kuipa Yanga bao, moja aliumiliki vizuri mpira akiwa eneo la Alger na kufumua shuti ambalo lilimbabatiza beki mmoja wa Alger na kuwa salama kwa timu hiyo.
Mzize hata hivyo alionekana akimlalamikia mwamuzi kwa madai kwamba mchezaji wa Alger aliyeokoa mpira huo aliunawa na hivyo kuonekana kama akitaka Yanga ipewe penalti.
Katika kipindi hicho hicho, Alger walifanya mashambulizi mawili tu ya maana langoni mwa Yanga, moja lilizaa mpira wa adhabu ambayo iliokolewa na kipa Djigui Diarra na la pili lilizaa kona baada ya Ibrahim Bacca kuokoa mpira akiwa ndani ya eneo la penalti wakati mshambuliaji wa Alger akiwa anaelekea kuonana na Diarra.
Kipindi cha pili, Yanga waliendelea na kasi yao ya kutafuta bao wakiwa tayari wamefanya mabadiliko kadhaa ikiwamo kumtoa Kennedy Musonda na nafasi yake kuingia Pacome Zouzoua.
Juhudi za mabeki wa Yanga akiwamo Shedrack Boca kupanda kusaidia mashambulizi hazikufua dafu mbele ya ukuta wa Alger ambao mabeki na wachezaji wake walio wengi ulitumia mbinu ya kujihami zaidi kadri dakika 90 zilivyokaribia kutimia.
Kwa ujumla kipindi cha pili Alger walilisogelea lango la Yanga mara chache, wakijihami zaidi na baadaye kutumia ujanja wa kupoteza muda, mbinu ambazo ziliwasaidi kupata matokeo ya sare yaliyowawezesha kufuzu hatua ya robo fainali.
Kimataifa Yanga yakwama Ligi ya Mabingwa
Yanga yakwama Ligi ya Mabingwa
Read also